×

“Tupinge Ukatili Wa Kijinsia, Mabadiliko Yanaanza na Mimi”

Maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia yameanza Novemba 25 ambapo yatadumu hadi Disemba 10, mwaka huu.

Wanaharakati mbalimbali wa masuala ya kupinga ukatili wa kijinsia hujitokeza na kufanya maandamano ya amani, lengo likiwa ni kufikisha elimu katika jamii.

Kaulimbiu ya mwaka huu ni; ‘Tupinge ukatili wa kijinsia, mabadiliko yanaanza na mimi’.

Akizungumza kwenye Semina za Jinsia na Maendeleo (GDSS) zinazoandaliwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Ofisa Program Idara ya Habari na Mawasiliano, Jackson Malangalila alisema kuwa, wao kama TGNP watakuwa na muendelezo wa kuwa na semina za GDSS ambapo masuala mbalimbali yatakuwa yakijadiliwa kuhusu ukatili wa kijinsia na kuendelea kutoa elimu kukomesha kabisa ukatili wa kijinsia.

Ofisa Program Idara ya Habari na Mawasiliano, Jackson Malangalila akizungumza na waliohudhuria.

“Tumejadili masuala mbalimbali ikiwemo uwekezaji (rasilimali fedha) katika mipango na mikakati ya kutokomeza ukatili.

“Tumewasikia wanajamii kwa pamoja, wametoa mawazo yao kwamba uwepo na bajeti ya kutosha endapo mhanga anapopata tatizo iwe rahisi kuchukuliwa na kufikishwa sehemu husika kwa haraka.

“Pia kuwepo na fungu ambalo litasaidia wanapofika hospitali mhanga aweze kupatiwa huduma mapema.

“Huduma zinazotolewa kwa wahanga wa ukatili wa kijinsia, mfano; kipindi cha Corona namna ambavyo zilikuwa zikitolewa na tumeona vile ambavyo wanajamii wamezungumza  kwamba kumekuwepo na changamto kuanzia Polisi hadi hospitali kama kuzungushwa kwa muda mrefu bila kupata huduma hivyo husababisha wengine kushindwa na kuacha watoto bila kupata huduma.

“Mikakati ya ulinzi kama inatosha ili matendo ya ukatili yasiweze kutokea, wanajamii wamezungumza namna ambavyo watoto na wanawake wanavyolindwa huko majumbani imeonekana kuna baadhi ya akina mama wanawaachia watoto bibi zao kwa kuwa uwezo wa bibi ni mdogo anashindwa kumlinda mtoto hivyo anajikuta akifanyiwa vitendo vya unyanyasaji ikiwemo kubakwa na mengineyo.

“Msisitizo katika kuzuia ukatili na unyanyasaji taarifa au takwimu zinazosaidia uboreshaji wa huduma za msaada kwa wasichana na wanawake hii itasaidia kujua idadi ya wahanga ili iwe rahisi kupata huduma.

“Tumetafakari kwa pamoja na wanajamii kuhusu namna wanavyoiona  mikakati ya kupinga ukatili wa kijinsia na pia wanajamii wamechangia kuwa kuna haja ya kuongeza nguvu zaidi katika rasilimali fedha katika mpango wa MTAKUWWA.

Wahudhuriaji wakisikiliza kiumakini.

“Wanajamii wametoa maoni yao kuhusu huduma kwa wahanga bado ni changamoto upande wa Polisi, hospitali na dawati maalum kwa hiyo uwepo uwezeshwaji ili wahanga waweze kupata tiba na ushauri mara moja ili kuwarudisha katika hali za kawaida,” alisema Jackson.

Katika maadhimisho hayo ya siku 16, wanajamii wamejipa majukumu ambavyo watakwenda kufanya ili na wao wawe sehemu ya mchango katika kupinga ukatili kwa kijinsia.

Kwa upande Kituo cha Taarifa na Maarifa Kata ya Mabibo jijini Dar wana mpango wao katika kupinga ukatili kwa akina mama na watoto kwa kuelimisha jamii kutoa taarifa mapema pindi matukio yanapotokea katika maeneo wanayoishi.

Kikundi cha sanaa kinachoitwa Munaa, wao wamekusudia kutunga wimbo wenye lengo la kutoa elimu kupinga ukatili kwenye jamii.

Agnes Lukanga kutoka Kituo cha Taarifa na Maarifa cha Kimara jijini Dar, alisema kuwa wameanza kutoa elimu kwa jamii maeneo yao kwa kupita na kuzungumza na watu mbalimbali.

“Tunapita kwenye vijiwe vya bodaboda, katika shule za msingi na sekondari kwa sababu siku hizi shule hizo zinajengwa maeneo ya pamoja hivyo watoto wadogo wa shule za msingi wanafanyiwa vitendo vya ukatili na watoto wa sekondari kwa kuwa wao wameshakuwa wakubwa, kuwapa elimu akina mama na akina baba wao huwa wanakuwa bize kiasi kwamba wanakosa muda wa kuwa karibu na watoto hivyo wajaribu kutenga muda wa kuwa karibu na watoto ili iwe rahisi kuwapa taarifa endapo watafanyiwa ukatili wa kijinsia iwe kubakwa na kulawitiwa,” alisema Agnes.

Mmoja wa wahudhuriaji akiuliza maswali kuhusiana na mada iliyokuwa ikiongelewa.

Kwa upande wa mchora-katuni wa magazetini, Msamba yeye mchango wake atachora katuni zinazolenga kutoa elimu na hamasa ili kuendelea kupunguza ukatilia wa kijinsia.

Kwa upande wa  mwanahabari, Yasmini Protas, yeye ataandika habari ambazo zitahabarisha jamii kuhusu ukatili wa kijinsia na kutoa elimu kwa jamii.

Maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia hufanyika kila mwaka kuanzia Novemba 25 hadi Disemba 10 ambapo wadau na mashikirika mbalimbali hutumia fursa hiyo kutoa elimu kwa jamii ili kutonyamazia aina zote za ukatili wa kijinsia.

Leave a Comment