×

Mtambo wa Mabao Watua Yanga SC

WAKATI Kocha wa Yanga, Cedric Kaze akiwa analia juu ya safu yake ya ushambuliaji kutokuwa namakali, leo Jumatatu anatarajia kuupokea mtambo wa mabao, Saidi Ntibazonkiza raia wa Burundi.

 

Ntibazonkiza ambaye alisaini mkataba wa miaka miwili kuitumikia timu hiyo tangu Oktoba, mwaka huu, alikuwa hajaungana na wenzake kambini kutokana na kuwa na majukumu ya timu ya taifa.

 

Hata hivyo, ilielezwa kuwa, jamaa huyo mwenye uwezo wa kucheza nafasi ya ushambuliaji na kiungo, alikuwa anasubiri dirisha dogo lifunguliwe ndiyo aanze kukipiga Yanga kumbuka usajili wa dirisha dogo unatarajiwa kufunguliwa Desemba 15, mwaka huu na kufungwa Januari 15, 2021.

Akizungumza na Spoti Xtra, Ofisa Habari wa Yanga, Hassani Bumbuli, alisema mapema leo Jumatatu, wanatarajia kumpokea Ntibazonkiza na kuanza mazoezi na wenzake akisubiri dirisha dogo lifunguliwe.

 

Ntibazonkiza anatarajia kutua hapa nchini Novemba 30, mwaka huu, kisha Desemba Mosi ataingia rasmi kambini kujifua na wenzake tayari kwa kuwania namba, ataanza kutumika mara tu dirisha dogo la usajili litakapofunguliwa Desemba 15, mwaka huu.

“Alitarajiwa kuwepo nchini tangu Novemba 18 mwaka huu, lakini kwa kuwa usajili wa dirisha dogo unaanza Desemba 15, ikabidi asubiri
kwanza.

 

“Taratibu zake za usajili kwa maana ya upande wa Shirikisho zitakamilika mapema tu ndani ya siku moja na atakuwa tayari kuwavaa wapinzani wetu ndani ya ligi,” alisema Bumbuli.

 

Ntibazonkiza ni mtambo wa mabao kweli akiwa ana uwezo wa kufunga kwa faulo za moja kwa moja ambapo alifanya hivyo katika mechi
za hivi karibuni akiwa na kikosi cha Burundi kwenye kufuzu michuano ya Kombe la Mataifa Afrika (AFCON).

 

Katika mechi za kufuzu AFCON zilizochezwa hivi karibuni, Ntibazonkiza alifunga mabao matatu, huku moja akifunga mechi ya kirafiki dhidi ya Tanzania, katika mabao hayo manne, mawili ni ya faulo za moja kwa moja dhidi ya Mauritania katika mechi ya kufuzu AFCON Kundi E.

Stori na MUSA MATEJA

 

Leave a Comment