×

Mugalu Ampa Matumaini Mapya Mbelgiji Simba

MAENDELEO mazuri ya straika wa Simba, Chris Mugalu, yamezidi kumpa matumaini kocha wa klabu hiyo Mbelgiji, Sven Vandenbroeck ambaye amesema anatarajia kumtumia straika huyo kwenye mchezo dhidi ya Mbeya City Jumapili hii.

 

Mugalu aliyefunga mabao matatu kwenye michezo minne aliyoichezea Simba kwenye ligi, amekuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu akiuguza majeraha ya nyonga aliyoyapata kwenye mazoezi ya kujiandaa na mchezo dhidi ya JKT Tanzania.

 

Majeraha hayo yamemfanya Mugalu akosekane kwenye michezo saba ya Simba, mitano ya ligi na miwili ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Plateau United ya Nigeria.

 

Akizungumzia hali ya straika huyo Sven alisema: “Tayari mshambuliaji wetu, Chris Mugalu ameanza mazoezi baada ya kuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu akiuguza majeraha ya nyonga, na sote tunakumbuka kuwa kutokana na majeraha hayo amekosa michezo saba.

 

“Kurudi kwake ni habari njema kwetu kwa sababu kunaongeza idadi ya washambuliaji waliokamilika ndani ya kikosi hasa kuelekea ratiba yetu ya michezo ya ligi kuu.

“Hivyo kama ataendelea kuimarika na jopo la madaktari likanihakikishia kuwa yupo sawa basi anaweza kutumika kwenye mchezo wa wikiendi dhidi ya Mbeya City.”

 

JOEL THOMAS, Dar es Salaam

Leave a Comment