
SPIKA wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai, amewataka mawaziri na naibu mawaziri walioapishwa leo Jumatano Desemba 9, 2020, kuwa na mahudhurio mazuri katika vikao vya bunge na kamati zake kwa kuwa ni takwa la kikatiba.
Ametoa kauli hiyo Ikulu ya Chamwino muda mfupi baada ya Rais John Magufuli kuwaapisha mawaziri hao aliowateua hivi karibuni.
Mbunge huyo wa Kongwa amesema kuhudhuria vikao hivyo isiwe kazi yake kuwakumbusha badala yake iwe ni wajibu wa kila mmoja.
“Haipendezi kuona waziri au naibu waziri wote hawapo katika kikao cha kamati au bungeni, mtambue kwenye vikao hivyo ndipo walipo wawakilishi wa wananchi lazima mkawasikilize,” amesema Ndugai.
Spika amewataka mawaziri hao kutolewa madaraka waliyopewa badala yake watambue kuwa wanalo jukumu kubwa la kuwatumikia Watanzania katika kumsaidia rais ambaye amebeba jukumu zito.
Amesema madaraka waliyopewa wateule hao ni lazima kila mmoja akafanye kazi akikumbuka kuwa inampasa kuweka alama ya nini alichokifanya.
Kwa mujibu wa Ndugai, viongozi hao wanatakiwa kwenda na dira ambayo ni Ilani ya CCM wakianzia na hotuba ya rais aliyoitoa wakati akilizindua Bunge.
Amesema viongozi hao ni wasaidizi wa kwanza wa rais aliyezunguka nchi nzima akibeba mzigo wa Watanzania, hivyo wanatakiwa kutopoteza imani hiyo waliyopewa ili ifikapo 2025 watu waone mabadiliko.