
KATIKA harakati za kupambana na ugonjwa wa Covid-19, #Kenya imeagiza dozi milioni 24 za Chanjo ya #CoronaVirus zitakazotosha 20% ya Wakenya.
Wizara ya Afya imesema dozi hizo zinagharimu Ksh. Bilioni 10 sawa na takriban Tsh. Bilioni 207.83, kiasi ambacho kitachangiwa na mataifa yaliyoendelea, hivyo kila dozi itagharimu Ksh. 320 sawa na Tsh. 6,600.
Katibu Mkuu wa Afya, Patrick Amoth, amesema wafanyakazi waliokuwa kwenye hatari ya kupata maambukizi pamoja na wazee watapatiwa chanjo hiyo.
Wizara iliwasilisha ombi lake kwa Mpango wa Ushirikiano wa Chanjo Duniani (Gavi) wiki iliyopita ambayo itawafikia asilimia ya 20 ya idadi ya watu nchini humo lakini haijabainika ni chanjo ipi iliyoagizwa na nchi hiyo ya Afrika Mashariki.
Kati kati ya mwaka huu Gavi ilisema kila dozi ya Covid-19 itagharimu Dola 3. Benki ya Dunia inakadiria kuwa Kenya wa sasa ina zaidi ya watu milioni 52. Waliorodheshwa kupewa chanjo ni wahudumu wa afya, wazee na wale waliyo na changamoto zingine za kiafya.
Gavi imetia saini mkataba na makampuni karibu tisa ya utengenezaji chanjo. Kenya inakuwa nchi iliyoagiza dozi nyingi zaidi kwa nchi za Afrika Mashariki. #Uganda iliagiza dozi milioni 9.