
KIONGOZI wa chama cha Wiper nchini Kenya, Kalonzo Musyoka hivi karibuni alitua katika Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC) katika juhudi za kuwapatanisha Rais Felix Tshisekedi na Rais mstaafu Joseph Kabila.
Uhasama baina ya wawili hao umekuwa ukitokota kwa miezi miwili sasa baada ya Tshisekedi kushikilia msimamo wake kuwa atavunja mkataba ambao alitia saini kwa siri kabla ya kukabidhiwa mamlaka ya nchi hiyo na Kabila Januari, mwaka jana.
Mkataba huo wa maelewano ulitiwa saini nyumbani kwa Kabila katika eneo la Kingakati jijini Kinshasa na kushuhudiwa na Rais Uhuru Kenyatta, Rais Abdel Fattah Sisi wa Misri na kiongozi wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa.
Kati ya mambo yaliyokuwa katika mkataba huo wa siri, ni kumtaka Rais Tshisekedi kumlinda Kabila pamoja na familia yake dhidi ya kushtakiwa kwa makosa ya mauaji au ufujaji wa rasilimali za umma.
Kabila pamoja na familia yake pia walitaka wapewe hadhi kubwa nchini DRC. Maelfu ya watu waliuawa kinyama na vikosi vya usalama wakati wa utawala wa Kabila aliyeongoza taifa hilo kati ya 2001 na 2019. Huenda Kabila alihofia kuwa angeshtakiwa baadaye kutokana na mauaji hayo.
Mwaka mmoja na nusu baada ya kutwaa hatamu za uongozi, Rais Tshisekedi ametangaza kutupa mbali mkataba huo huku akisema kuwa sheria ni lazima ifuate mkondo wake.
Tshisekedi amekuwa alisisitiza kuwa yuko tayari kuvunja bunge na kuandaa uchaguzi mpya iwapo hatapata chama cha kufanya muungano nacho kuendesha serikali.
Katika hotuba yake aliyoitoa Disemba 20 mwaka huu, Rais Tshisekedi ameyagusia masuali mengi ambayo amesema yalijitokeza katika mazungumzo yaliyofanyika Novemba kuhusu mustakabali wa muungano huo.
Aliongeza baada ya mazungumzo hayo jambo l a muhimu zaidi lilikuwa ni hatua za kuhitimisha ushirikiano baina ya muungano wa vyama vinavyomuunga mkono yeye, maarufu CACH, na ule wa vyama vilivyo upande wake rais mstaafu Joseph Kabila yaani FCC.
“Nimeamua kumaliza ushirikiano kati ya FCC na CACH. Hatua hiyo ya kusikitisha imekuja baada ya kujaribu muda wa miaka miwili, kusubiri na kuvumilia ili kuunusuru ushirikiano huo. Miaka miwili ya juhudi ila kwa kweli, hatukufaulu kuepuka hali ya vurugu iliyodumu,” alisema Rais Tshisekedi.
Chama kinachodhibitiwa na Kabila kina wabunge 300 kati ya 500 walio katika bunge la DRC. Wabunge hao wote 300 wa Kabila walikuwa wakiunga mkono Tshisekedi kabla ya uhusiano wake nyongo.na Kabila kutumbukia
Kabila tayari ameandikia barua Umoja wa Afrika (AU), Marais Kenyatta, Sisi na Ramaphosa akiwataka kuingilia kati na kumshawishi Rais Tshisekedi kuzingatia mkataba waliotia saini.
RAILA NA KENYATTA
Kabla ya kutangaza rasmi ushirikiano wao mnamo Machi 2018, Rais Kenyatta na kiongozi wa chama cha ODM, Raila Odinga walifanya ‘mkataba’ wa siri ambao haujawahi kuwekwa wazi.
Mara baada ya kutangaza kushirikiana, Rais Kenyatta na Odinga walianza mchakato wa Mpango wa Maridhiano (BBI) ili kurekebisha Katiba.
Odinga amekuwa katika mstari wa mbele ‘kusukuma’ BBI. Lakini Odinga anameonywa kujihadhari ili asije akaachwa kwenye mataa baada ya kupitishwa kwa mswada wa BBI.
Kama wasemavyo Waswahili: mwenzako akinyolewa, chako tia maji. Siasa ni mchezo mchafu uliosheheni usaliti.
GABRIEL MUSHI NA MITANDAO