×

Marekani: Trump Apigwa Kotekote

CHAMA cha Democratic cha rais mteule, Joe Biden, sasa kina udhibiti wa mabunge yote mawili ya Marekani baada ya kuibuka na ushindi wa viti viwili vya Seneti.

 

Democrat kimenyakua viti hivyo katika uchaguzi wa marudio jimbo la Georgia. Viti hivyo vilikuwa chini ya mahasimu wao chama cha Republican muhula uliopita. Hili ni pigo kubwa la kisiasa kwa rais anayeondoka madarakani, Donald Trump, wa Republican.

 

Kwa mara ya kwanza toka mwaka 2009 chama cha Democrat kitakuwa na udhibiti wa Ikulu ya White House, Bunge la Wawakilishi (Congress) na Bunge la Juu (Seneti). Takriban watu milioni nne walijitokeza kupiga kura katika uchaguzi wa marudio jimboni Georgia.

 

Uchaguzi huo wa Maseneta ulilazimika kurejewa kwa kuwa hakuna aliyefikia asilimia 50 ya kura ulipofanyika uchaguzi mkuu Novemba 2020. Sasa Raphael Warnock na Jon Ossoff wamewashinda Maseneta waliokuwa wakitetea viti vyao Kelly Loeffler na David Perdue.

 

Warnock, ambaye ni mchungaji wa kanisa la Baptist, anakuwa seneta wa kwanza mweusi wa Georgia, jimbo ambalo liliingia katika vita ya wenyewe kwa wenyewe ya Marekani ikitaka utumwa uendelee. Pia anakuwa seneta wa 11 mweusi katika historia ya Marekani.

 

 

Je, matokeo haya yana maana gani?

Kwa matokeo ya Georgia, Democrat na Republican wote watakuwa na viti 50 katika Bunge la Seneti. Hata hivyo, Makamu wa Rais Ajayi kutoka Democrat, Kamala Harris, ataongoza wenzake katika Bunge la Seneti na atakuwa na kura ya ushindi kwenye mijadala.

 

Hali hiyo itaupa uongozi wa Biden nafasi kubwa ya kutekeleza ajenda zake zikiwemo huduma za afya na mabadiliko ya tabianchi. Seneti pia ina nguvu ya kupitisha ama kuwakataa wateule wa  Biden katika nafasi za mawaziri na mahakama.

 

Je kinyang’anyiro kilikuwaje?

Ushindani ulikuwa mkubwa katika uchaguzi wa viti vyote viwili. Mchungaji Warnock amepata 50.7% dhidi ya 49.3% alizopata Seneta Kelly Loeffler ambaye ni mfuasi mkubwa wa Trump.

 

Katika kiti cha pili ushindani ulikuwa mkubwa zaidi. Jon Ossoff amepata 50.28% dhidi ya 49.72% alizopata Seneta David Perdue, 70. Rais Trump anaendelea kutoa madai yasiyokuwa na ushahidi ya wizi wa kura, huku akitilia mashaka uhalali wa uchaguzi wa Georgia.

 

Trump amesikika katika mkanda wa sauti uliovuja siku ya Jumapili akimshinikiza afisa wa juu wa uchaguzi wa jimbo hilo, Brad Raffensperger, ambaye pia ni mwanachama wa Republican, “kutafuta” kura za kutosha ili kupindua ushindi wa Biden katika jimbo hilo.

Leave a Comment