
Hadija Said mkazi wa Kimara Kwa Mtoro Bonyokwa jijini Dar ambaye anayedaiwa kuishi katika mazingira magumu baada ya kifo mumewe na kuelemewa na familia, amesaidiwa mahitaji mbalimbali ikiwemo pesa ya mtaji na Wanawake wanaounda Kundi la Share Meal and Give Capital.

Msafara wa Wanawake hao ukiongozwa na Mwenyekiti wao Catherine Ambakisye maarufu Mama Rolaa ulifika nyumbani kwa mwanamke huyo na kumpatia vitu mbalimbali ikiwemo vyakula, mafuta, sabuni na mahitaji mengine. Kinamama hao pia walimpatia kiasi fulani cha pesa kwa ajili ya kuanzisha biashara ndogondogo ya kujikimu.

Baada ya kupewa msaada huo Bi. Hadija aliwashukuru wanawake hao na kuwaombea baraka kwa Mwenyezi Mungu na kuwaomba Wasamaria wema wengine kumsadia ili aweze kuishi na watoto watatu ambapo mmoja amefaulu kuingia kidato cha kwanza mwaka huu lakini amekumbana na kikwazo cha sare za shule madaftari na mengineyo.

Mwanamke huyo ameomba kama kuna Wasamaria wema wengine wamsaidie kupitia namba yake ya simu ya mkononi 0658638684 jina la usajili Hadija Said.

Naye Mjumbe wa Shina wa eneo hilo Gaspar Ntokwa baada ya kushuhudia msaada huo ukitolewa aliwashukuru kinamama wanaounda kundi hilo na kuwaomba msaada wao usiishie hapo uwaangalie na wengineo kwa maana wenye shida kama hizo wape wengi sana na atawalipa kwa jinsi wanavyojitolea.

“Huyu mama ni mkazi wangu hapa mtaani namfahamu anavyoishi katika mazingira magumu tangu alipofiwa na mumewe na kumuachia watoto watatu hata hapa anapoishi kuna Msamaria mwema ndiye amemuhifadhi.

Hivyo msaada wenu una maana kubwa sana kwake na hata kwangu kama kiongozi wa eneo hili analoishi huyu mama”. Alimaliza kusema mjumbe huyo.
HABARI/PICHA: RICHARD BUKOS /GPL