
Kocha wa zamani wa Yanga, Mwinyi Zahera, raia wa DR Congo, amefunguka kuwa anaamini Simba itafika mbali katika Ligi ya Mabingwa Afrika kutokana na ubora wa wachezaji wake wakiwemo Mzambia, Clatous Chama na Mnyarwanda, Meddie Kagere.
Zahera ametoa kauli hiyo kufuatia Simba kuanzisha michuano ya Simba Super Cup ambayo itashirikisha timu tatu ambazo ni TP Mazembe ya DR Congo na Al Hilal ya Sudan kabla ya kuanza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo Simba imepangwa Kundi A ikiwa na Al Ahly ya Misri, As Vita ya DR Congo na Al Merreikh ya Sudan.
Akizungumza na Championi Jumatatu, Zahera alisema kuwa ubora wa wachezaji wa Simba wakiwemo Chama na Kagere utasaidia katika michuano hiyo kutokana na kupata bahati ya kukutana na timu inazozifahamu vizuri.
“Simba itafika mbali Ligi ya Mabingwa kwa sababu wachezaji wengi wana uwezo wa michuano yenyewe lakini bahati ya kukutana na timu ambazo walishacheza nazo katika hatua hiyo, hivyo ni suala la wao wenyewe kujipanga vizuri.
“Mtu kama Chama, Kagere au Bocco (John) wote wameshacheza msimu mmoja uliopita na walifanya vizuri, unadhani safari hii nini kitatokea na ikizingatiwa wamesajili wachezaji halafu tena wanamichuano ya Simba Super Cup, itawasaidia nakwambia maana inaenda kushangaza Afrika,” alisema Zahera.
Ibrahim Musa | Championi