×

Watu Zaidi ya 60 Wafariki Dunia Ajali ya Boti

WATU zaidi ya 60 wameripotiwa kufariki dunia baada ya boti waliokuwa wakisafiria kupinduka na kuzama katika mto Congo nchini Jamhuri ya Kidemkokrasia ya Congo (DRC).

 

Maofisa wa Polisi Usalama nchini humo wamesema watu wengine 300 wameokolewa lakini inakisiwa kuwa watu 200 hawajulikani walipo mpaka sasa baada ya ajali hiyo. Wakazi wanasema boti iligonga mwamba mashariki mwa mji mkuu Kinshasa, wakati walipokuwa wakisafiri usiku.

 

Imeelezwa kuwa safari za majini nyakati za usiku zimepigwa marufuku nchini humo. Waziri wa Masuala ya Kibinadamu, Steve Mbikayi, amewataka wamiliki wa boti hiyo kushtakiwa.

 

“Chombo kilichojaa kupita kiasi, kilichokuwa na abiria zaidi ya 700 kilipinduka Mai-Ndombe! Miili 60 tayari imepatikana na watu 300 wamenusurika. Tunazipa pole familia zilizofiwa na tunataka hatua zichukuliwa dhidi ya wale wote wanaohusika na sekta ya uchukuzi,” aliandika waziri huyo kwenye mtandao wa Twitter.

 

 

Kuna barabara chache nchini DRC na shughuli nyingi za usafirishaji wa mizigo na abiria hufanywa kwa njia ya mito.

Leave a Comment