
TUMUOMBEE!Ndivyo walivyosikika baadhi ya waombolezaji waliokuwa kwenye ibada ya mazishi ya Hayati Dk John Pombe Magufuli kwenye Uwanja wa Magufuli, Chato mkoani Geita, jana.
Waombolezaji hao waliyasema hayo mara baada ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Kassim kueleza kuwa mama mzazi wa Hayati Magufuli bado anaumwa na Serikali itaendelea kumhudumia.
“Jamani tumuombee bibi yetu ili aweze kupona maana ni muda mrefu sasa anaumwa si chini ya miaka miwili sasa yupo kitandani,” alisikika mmoja wa waombolezaji ambaye aliungwa mkono na waombolezaji wengine.

Waziri Majaliwa alisema mama huyo mzazi wa Hayati Rais Magufuli bado ni mgonjwa na yupo kitandani kwa miaka miwili.“
Nimeongea na Mh. Rais kuhusiana na jambo hili na tutahakikisha madaktari wanamtibu bibi yetu hadi pale atakaporejea katika hali yake ya kawaida,” alisema Majaliwa.

Waziri Majaliwa alisema, msiba huo umewagusa Watanzania wengi na kama Taifa hawana budi kumshukuru Mungu na kumuenzi Hayati JPM kwa vitendo.
Pia aliwashukuru wasanii, waandishi wa habari na Watanzania kwa ushirikiano waliouonesha katika kipindi chote cha maombolezo.
STORI: MWANDISHI WETU