
KUELEKEA mchezo wao wa leo Ijumaa katika Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly, uongozi wa Klabu ya Simba umelazimika kuwaongezea ulinzi nyota wa kikosi chao hasa Luis Miquissone na Clatous Chama ambao wameonekana kusakwa tangu kikosi chao kilipotua.
Taarifa za kuaminika kutoka chanzo cha karibu na Simba zinasema kuwa tangu walipotua kwenye Uwanja wa Ndege wa Cairo, juzi Jumatano, wakazi wengi wa Jiji la Cairo wamekuwa wakitafuta nafasi ya kuwaona wachezaji wa Simba huku Luis na Chama wakionekana kuuliziwa zaidi.
Nyota hao wawili wiki iliyopita walichaguliwa kuingia ndani ya kikosi bora cha Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuhusika katika mabao yote manne waliyoyapata katika ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya AS Vita, ambapo Chama pia alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa wiki wa michuano hiyo.

Akizungumza na Championi Ijumaakuhusu maendeleo ya kambi yao meneja wa kikosi cha Simba, Patrick Rweyemamu alisema: “Kambi ya kikosi chetu iko salama kabisa, na kila kitu kuhusu ulinzi na hali za wachezaji kuelekea mchezo wa kesho (leo) viko vizuri, na tunaendelea vizuri na maandalizi ya mwisho.
“Tunajua tunakwenda kucheza dhidi ya timu ngumu lakini, tuwatoe hofu mashabiki wetu kwamba tutapambana kuhakikisha tunapata matokeo mazuri kwa kuwa tumekiandaa kikosi chetu kupata matokeo kwenye mazingira yoyote.
”Simba inaongoza msimamo wa Kundi A kwa kuwa na pointi 13 katika ligi hiyo, ikifuatiwa na Al Ahly wenye pointi 8 huku timu zote mbili zikiwa zinaingia katika mchezo huo zikiwa tayari zimefanikiwa kutinga hatua ya robo fainali.
STORI: JOEL THOMAS, CHAMPIONI