×

Rais Samia: Makosa Sio Kitega Uchumi cha Polisi – Video

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amelitaka jeshi la polisi kujielekeza zaidi kutoa elimu badala ya kutumia sheria zao kutoza faini. Pia amelitaka jeshi hilo kuwa na mfumo utakaosomeka nchi nzima na kuonesha makosa ya madereva, na yakifika kiwango fulani, dereva anyang’anywe leseni.

 

Rais Samia amesema hayo leo Mei 18, 2021 wakati akizindua kiwanda cha ushonaji cha jeshi la polisi kilichopo kilichopo katika Bohari Kuu ya Jeshi la Polisi Kurasini jijini Dar es Salaam.

 

“Takwimu zinasema kuna upungufu wa makosa na upungufu wa makusanyo ya pesa kutokana na upungufu wa makosa, nataka nielekeze kwamba kazi ya Jeshi la Polisi ni kudhibiti makosa, tusijielekeze sana kwenye kipengele makosa na adhabu kwamba ni kitega uchumi, zaidi zitumike kudhibiti kuliko ukusanyaji wa faini na tozo nyingine. Nihimize suala la elimu kwa raia, naona vipindi vyenu kwenye TV lakini naomba muongeze zaidi.

 

“Baada ya kutoa ile kauli yangu kuhusu wahalifu IGP ulifanya mkutano na kuweka mikakati, lakini tunasikia bado kuna wanaojaribu kina cha maji, wanabonyeza bonyeza, nawaomba mjipange, wakibonyeza pasibonyezeke, kama mliweza huko nyuma hamuwezi kushindwa sasa.

 

“Kuna mambo yanashangaza kulikuwa na sheria wote tusajili laini tuweke vidole ili mtu akifanya utapeli ajulikane lakini utapeli wa mtandao unaendelea na watu hawafikishwi mahakamani, sasa ule usajili ulikuwa kiini macho au nini? Maana wote tumesajili na majina yapo.

 

“Hii sio kwa Dar es Salaam tu, bali nchi nzima, miongoni mwa vigezo tutakavyovitumia kuteua au kutengua Makamanda wa Polisi wa Mikoa ni kasi ya kudhibiti vitendo vya uhalifu, kwahiyo mkajitahidi kudhibiti vitendo vya ujambazi,” amesema Rais Samia.

 

Awali, Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania (IGP) Simon Sirro amesema kiwango cha makusanyo ya faini za makosa ya Barabarani kimepungua kwasababu Watu wengi sasa wanaanza kuwa watii; “Mwaka jana July 2019 na July 2020 jumla ya Tsh. Bilioni 56 zilikusanywa lakini sasa kiwango kimepungua.” 

 

Leave a Comment