×

Kaseke Aibeba Yanga, Yatinga Nusu Fainali ASFC

TIMU ya Yanga imefanikiwa kufuzu hatua ya nusu fainali ya michuano ya kombe la shirikisho (ASFC) baada ya leo kuilaza Mwadui FC mabao 2-0.

 

Katika mchezo huo uliopigwa uwanja wa Kambarage mjini hapa, Yanga walionekana kuimarika zaidi ya wapinzani japokuwa safu ya ushambuliaji ilikosa makali kutokana na kushindwa kutumia vyema nafasi walizopata.

 

Katika kipindi cha kwanza Yanga waliutawala zaidi mchezo kwa mashambulizi ya hapa na pale ambayo hayakumpa raha Kipa wa Mwadui, Mussa Mbisa na kujikuta akifungwa dakika ya 25 na Deus Kaseke huku akiokoa hatari nyingi.

 

Kipindi cha pili Kaseke tena aliweza kucheka na nyavu dakika ya 57 alipomtungua vyema Mbisa, bao ambalo lilidumu hadi dakika 90 zinamalizika na kuihakikishia timu yake kufuzu hatua hiyo.

 

Hata hivyo Mwadui walipambana kipindi cha pili kusaka mabao lakini hatari zote ziliishia mikononi mwa Kipa Shikhalo na nyingine mabeki wakiongozwa na Mwamunyeto wakifanya kweli kwa kuondosha mipira iliyoelekezwa kwao.

 

Pia timu zote zilifanya mabadiliko ambapo Yanga iliwatoa Nchimbi na Kaseke na kuwaingiza Waziri Junior dakika ya 70 na Farid Mussa dakika ya 83.

 

Mwadui nao walimtoa Feisal Rajab na kumwingiza Deogratius Anthony dakika ya 66 mabadiliko ambayo hayakubadili chochote katika dakika hizo.

Leave a Comment