
Na Mwandishi Wetu
MSANII anayefanya vizuri katika tasnia ya muziki wa kizazi kipya nchini Nigeria, Idahams amefanikiwa kukivuka kikwazo cha maradhi ya Covid-19 kwa kuachia albamu maalum (Extended Play- EP) iitwayo ‘Man On Fire’ yenye jumla ya nyimbo saba zilizobeba ujumbe wa kuwafariji na kuwapa moyo watu wote katika kipindi hiki kigumu ambacho dunia inapambana na Janga la Corona.
Nyimbo zilizomo ndani ya albamu hiyo ni mchanganyiko wa aina mbalimbali za muziki ikiwemo Afro Pop, Rap na aina nyingine hususan unaopatikana barani Afrika, ukiwemo wimbo wa Ada na Man on Fire alizoshirikiana na mwanamuziki mwingine, Falz, Shima alioshirikiana na Peruzzi na Seyi Shay.
Katika albamu hiyo, Idahams anaendeleza moto aliouwasha mwaka 2020 kwa kutoa nyimbo kali zaidi ya zile zilizopo kwenye albamu yake iliyopita kama Belle, God When na No One Else alioutoa mwaka 2018 ambao ulisababisha asainiwe na lebo kubwa za Universal Music na Grafton Records.
Ndani yake, Idaham ameendelea kuonesha uwezo mkubwa wa namna anavyoweza kutunga nyimbo zenye mashairi mazito, zilizoandaliwa na maprodyuza bora kwa kuzingatia asili yake ya Kusini mwa Nigeria sambamba na midundo mizuri inayomfanya kuendelea kuwa msanii tishio barani Afrika.

Akizungumzia mafanikio ya kukamilika kwa EP hiyo, Idahams ambaye amesaini kwenye Lebo ya Universal Music and Grafton Records, anasema: “Niliamua kuongeza nyimbo tatu kwenye EP yangu ya 2021 ya Deluxe kwa sababu nilihisi kuwa mwaka huu mashabiki wangu wanapaswa kuwa na zaidi kutoka kwa toleo la asili la EP ya ‘Man On Fire’ ya 2020.
“Jibu ni kwamba imekuwa kubwa na ninaweza kuona mashabiki wakiwa wabunifu wa nyimbo. Hii inafanya mradi wangu mkubwa kwa sasa. Najivunia sana hili kwa kweli.”
Aidha, anasema katika mipango yake ya mwaka huu ni pamoja na kufanya kazi na msanii wa Bongo Fleva, Diamond Platnumz ambaye amesema kwake, ndiye msanii anayeona ana uwezo mkubwa zaidi.
“Nafuatilia kazi za Diamond. Ni msanii mzuri, anajua kuimba, midundo mizuri na kwa kweli nikishirikiana naye kuna kitu kikubwa nahisi nitakivuna kwake, naye pia kwangu,” anasisitiza Idahams.