
SERIKALI imesema maamuzi kuhusu chanjo ya virusi vya corona hapa nchini hayajafikiwa kama baadhi ya watu wanavyodai kutokana na kauli ya Rais Samia Suluhu ya jana alipopokea taarifa ya kamati maalum aliyoiteua kwa ajili ya kuishauri serikali kuhusu janga hilo.
Hayo yamesemwa leo Jumamosi, Juni 5, 2021 na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma na kueleza utendaji kazi wa Serikali ya awamu ya sita ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Tunashukuru njia tunazotumia kukabiliana na janga hili zimetusaidia hatujapata madhara makubwa sana kama nchi nyingine, pamoja na kufuata miongozo iliyoloewa na Shirika la Afya Duniani (WHO), Mhe Rais aliamua kutumia watalaam wetu wa ndani kufanya tafiti za namna ya kukabiliana na huu ugonjwa kisha kuishauri Serikali nini cha kufanya ili kuepuka madhara ya janga hilo.
“Timu ya wataalam imefanya kazi iliyokuwa imegawanyika katika sehemu mbili, kwanza na wametoa ripoti ya mapendekezo yao kuhusu nini kifanyike, na jana wamewasilisha mpango kazi wa namna ya upatikanaji wa rasilimali ya kukabiliana na hili janga, pia mpango kazi wa namna ya kupata chanjo.
“Kamati maalum ya Corona watalaam wameshawasilisha mapendekezo kwa Rais ambaye ameagiza Wizara ya Afya iandike andiko, litapekekwa Baraza la Mawaziri watajadili na kushauri kisha Serikali itatoa tamko, haina maana kwamba maamuzi, hapana.
“Kwa hiyo yale maneno ya kwamba labda serikali imelegeza hapana, tusikilize serikali na hatua ambayo serikali imechukua ili tubaki salama kwa ajili ya afya zetu na uchumi wetu. Tunao watalaam wa kustosha.
“Yako maeneo ambayo imebidi serikali ifanye maamuzi kama kuruhusu balozi na taasisi za kimataifa kuingiza chanjo kwa sababu nchi yetu ina balozi ambazo zina raia wao, na kwenye nchi zao tayari wanachanjwa, hivyo baadhi ya shughuli zao hawafanyi kwa sababu hawajachanjwa.
“”Mpango wa chanjo kwa Watanzania wengine utasubiri maamuzi ya serikali baada ya hatua hizi ambazo Mhe Tais ameagiza. Watanzania tuendelee kuchukua tahadahari kwa sababu ugonjwa huu upo,” amesema Msigwa.