
RAIS mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete amesema sera ya kukuza uchumi na kujenga viwanda ilikuwa ni dira aliyoitengeneza na kuanza kuitekeleza rais wa awamu ya tatu, hayati Benjamin Mkapa.
Kikwete amesema hayo leo Jumatano, Julai 29, 2020, katika Kijiji cha Lupaso, Masasi mkoani Mwtara wakati wa maziko ya Mkapa.
“Ni ngumu kupata maneno ya kumuelezea Mzee Mkapa, nimemfahamu miaka mingi, tangu nikiwa mwanafunzi lakini kwa mara ya kwanza nimefanya naye kazi nilipokuja kuwa Katibu wa CCM wa Wilaya ya Masasi yeye akiwa Mbunge wa Nanyumbu, alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje ila pamoja na ubize aliwatumikia wananchi.
“Wilaya hii ya Masasi ilikuwa na tatizo la njaa wakati ule, nikiwa Masasi na DC tukabuni mradi wa kilimo cha muhogo ambacho hakikupendeza sana kwa sababu Wamakua hawapendi sana kula ugali wa mihogo kama mashemeji zangu Wamakonde, ila Mzee Mkapa alisimama nasi.
“Yeye alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje na muda mwingi yuko angani, kwa hiyo tabu unayoipata ni namna ya kulilea jimbo, lakini jambo alilokuwa analifanya kila alipopata nafasi, hakuacha kuja kwenye jimbo na mimi nilikwa najuimuika naye kwenye mizunguko yake.
Wakati nikiwa rais, Mzee Mkapa alikuwa akinipigia simu bila hata kusubiri mimi kuuliza, alinisaidia sana masuala mengi nikiwa rais. Mzee Mkapa alikuwa mtu wa mikakati, alipenda kusaidia watu kutoka katika umasikini, aliweka mipango na mikatikati kutekeleza hilo. Dira ya uchumi wa kati ni ya Mkapa.
“Sera ya viwanda ya sasa ni sehemu ya mpango mkakati wa dira ya uchumi wa Tanzania kufikia uchumi wa kati, kwa sasa serikali inapotekeleza sera ya viwanda ni mikakati ya Mzee Mkapa. Alinipa wizara kubwa sana ‘Wizara Mambo ya Nje” ingawa nilishindana naye kwenye urais, hakuniweka mbali, hakutaka nipotee kama zilivyo siasa zetu za sasa mtu uliyeshindana naye.
“Rais Mkapa alikuwa anachukia sana suala la umaskini, yeye ndiye alitengeneza dira ya mwaka 2025, iwe nchi ya uchumi wa kati na pato la wastani wa Mtanzania iwe dola 3,000. Tumeshafika kwenye uchumi wa kati lakini hatujafika kwenye lengo lile ambalo Mzee Mkapa alilikusudia, bado sana kama dola 2,000 hivi, mimi naamini mkimpa nafasi Mzee Magufuli tutafika kule.
“Mzee Mwinyi amepokea Tanzania uchumi wa nchi ukiwa katika mazingira magumu, amefanya jitihada kuuinua, Mzee Mkapa akaipokea nchi uchumi ukiwa bado, akapigana sana na kipindi chake cha miaka mitano ya mwisho uchumi wa Tanzania ukawa unakuwa kwa 7%.
“Na mimi nikasema lazima nihakikishe uchumi unakuwa kwa asilimia saba katika kipindi changu, ndivyo nilivyofanya kwa miaka yangu yote ya uongozi, nikamwachia Mheshimiwa Magufuli naye anapambana na anajitahidi kuupandisha uchumi wetu.