
KATIBU mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesikitishwa na mauwaji ya raia kaskazini mwa Burkina Faso, maafisa wa Burkina Faso wamesema watu wanaoshukiwa kuwa wapiganaji wenye msimamo mkali wa kidini wamewauwa watu wapatao 138 katika mashambulizi mabaya zaidi kuwahi kufanywa tangu machafuko yalipozuka nchini humo mwaka 2015.
Stephane Dujarric msemaji wa katibu mkuu wa Umoja wa mataifa, amesema, Guterres ameghadhabishwa na mauaji ya watu hao wakiwemo watoto 7.
Mauaji hayo yamefanywa na watu wasiojulikana katika kijiji cha Solhan kilicho katika mkoa wa Yagha eneo la Sahel nchini Burkina Faso.
Rais wa Burkina Faso Roch Marc Christian Kabore amelaani vikali shambilizi hilo karibu na mipaka wa Mali na Niger ambako wapiganaji wa jihad wenye mafungamano na mtandao wa kigaidi wa Al-Qaeda na kundi linalojiita dola la kiisalam wamekuwa wakiwashambuilia raia na wanajeshi.