The House of Favourite Newspapers

Humud ageuzwa beki Coastal Union

0

HumudBAADA ya Tumba Sued kutimkia Mbeya City, Coastal Union sasa ipo katika harakati za kumbadili kiungo wake, Abdulhalim Humud ili acheze beki ya kati iliyokuwa ikichezwa na Tumba.

Humud aliyewahi kutamba akiwa na Ashanti United, Simba, Azam FC na Taifa Stars, anamudu kucheza nafasi ya kiungo mkabaji na mshambuliaji kwa muda mrefu.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Coastal Union, Salim Bawaziri, timu yake itasajili wachezaji wanne tu katika kipindi hiki cha usajili wa dirisha dogo, lakini haitasajili beki.

“Tumba ameondoka na hakika hatutasajili beki mwingine kuziba nafasi yake, badala yake tutamtumia Humud kucheza nafasi hiyo akisaidiana na mabeki wengine Hamis Kibacha na Yusuph Chuma.

“Tunafahamu si kazi rahisi lakini ni jukumu la mwalimu kuweza kulitimiza hilo na nafasi hii tumempa baada ya hivi karibuni kurejea rasmi klabuni na kuungana na wenzake,” alisema Bawaziri.

Humud tangu aliposajiliwa amekuwa na matatizo mbalimbali na kuna wakati alitoweka bila ruhusa na aliporejea alitakiwa kuomba msamaha ndipo aliporejeshwa kikosini.

Leave A Reply