ILIPOISHIA IJUMAA:
Wakati dereva analiwasha gari hilo na kuliondoa, mawazo yakaanza kunijia. Nilijiuliza hao polisi walitaka kunihoji kuhusu nini na mke wangu walitaka kumhoji nini?
Wasiwasi wangu ulikuwa ni endapo gari langu lilionekana nilipoliegesha wakati nilipokwenda kumuwangia waziri mkuu.SASA ENDELEA…
Nilijiambia kama litakuwa limeonekana, lazima polisi watakuwa wananingoja kwa hamu kunihoji.Nikaendelea kujiambia pengine wale polisi walionikurupusha nyumbani kwa waziri mkuu wametoa taarifa kwa wenzao juu ya vitendo nilivyofanya kando ya mlango wa nyumba ya waziri mkuu.
Nikazidi kupata hofu nilipowaza kuwa huenda yule polisi aliyeniona nikikita kimba nitamkuta kituo cha polisi ambako ameambiwa asubiri ili anitambue.
Nilijiambia kama itakuwa hivyo ni bora nisiende polisi.
Lakini nikajiuliza nisipokwenda itakuwaje, si ndiyo nitakuwa mshukiwa na sitaweza kujitetea kwa lolote.Nikaamua niende ingawa nilikuwa na tumaini dogo la kutoa maelezo yanayoweza kukubalika.
Gari lilipofika kituo cha polisi nikaliona gari langu lililokuwa limekamatwa. Lilikuwa limeegeshwa mbele ya kituo hicho cha polisi. Nilifungua mlango wa gari nililokuwa nimepanda nikamwambia dereva wangu anisubiri.
Wakati nashuka nilimuona dereva wa mke wangu naye akiwasili kwa pikipiki.
Nilisimama kumsubiri. Alishuka kwenye pikipiki akanifuata.
“Gari lenyewe lile pale,” nikamwambia.
Dereva huyo akalitupia macho.
“Loh! Jamaa walitaka kulichukua.”
“Lakini wamelikosa. Jana usiku sikulala kwa raha na nilishindwa hata kumueleza mke wangu.”
“Lazima ukose raha, gari bado jipya kabisa.”
“Hebu twende tukawasikikize hawa mabwana.”
Nikafuatana na yule dereva kuelekea kwenye lango la kituo cha polisi.
Tuliingia ndani ya kituo hicho. Ingawa ilikuwa asubuhi tayari polisi walikuwa katika pilikapilika za kikazi.
Tulikwenda kaunta nikajieleza kwa mmoja wa polisi waliokuwa hapo.
“Oh! Mkuu wa kituo alikuwa anakusubiri. Twende nikupeleke ofisini kwake.
Wakati nafuatana na yule polisi nilimwambia yule dereva wa mke wangu.
“Twende.”
“Na huyo ni nani?” yule polisi akaniuliza.
“Ni dereva wangu.”
“Ndiye aliyekuwa akiendesha lile gari unalosema limeibwa?”
“Hapana.”
“Basi acha akusubiri hapahapa.”
“Sawa.”
Dereva huyo akabaki hapohapo. Nilipelekwa katika ofisi ya mkuu wa kituo. Yule polisi aliyenisindikiza akatoka.
Mkuu wa kituo hicho alikuwa mtu mzima aliyekaribia umri wa kustaafu.
Kwa vile mimi nilikuwa kijana sana kwake nilimwamkia.
“Shikamoo?”
“Marahaba. Karibu kiti mheshimiwa,” akaniambia huku akinitazama kwa macho ya udadisi.
Nilishuku pengine alikuwa akijiuliza kama kweli mimi naweza kuwa mchawi.
Nikakaa kwenye kiti kilichokuwa mbele ya meza yake.
“Umefanya vizuri, umefika mapema. Tulitegemea kukuona ukiwa na mke wako kama tulivyokueleza,” mkuu huyo wa kituo akaniambia.
“Mke wangu ni mgonjwa amekwenda hospitalini.”
“Si ulituambia kuwa ulikuwa naye jana usiku kabla ya gari lenu kuibwa?”
Mara nyingi ukitaka kusema uongo kumbuka kutokuwa msahaulifu. Nilishasahau kuwa nilisema hivyo.
“Ndiyo. Nilisema hivyo lakini ameamka hii asubuhi akiwa hajisikii vizuri. Amekwenda kupima kujua kama ana malaria.”
“Sawa. Gari lako umeliona hapo nje?”
“Ndiyo nimeliona.”
“Ndiyo hilo?”
“Ndiyo lilelile.”
Mkuu huyo wa kituo alinyamaza kimya kidogo akatazama pembeni kama aliyekuwa anafikiri kitu kisha akaniambia.
“Kumekuwa na matukio mawili tofauti kuhusiana na lile gari. Tukio la kwanza, lile gari liliwakimbia polisi usiku liliposimamishwa.
Polisi wakalitilia shaka na kuamua kulifukuza. Lakini hawakulipata usiku ule.
“Alfajiri ya leo gari hilo lilikutwa limeegeshwa sehemu likiwa halina mtu. Polisi wakalikamata. Tulipolipekua tulikuta likiwa na kadi iliyokuwa na jina lako. Kadi yenyewe ni hii hapa.”
Mkuu huyo wa kituo alinionesha kadi ya gari langu iliyokuwa juu ya meza yake.
Nilipoitazama niligundua kweli ilikuwa kadi ya gari langu.
“Tukio la pili linalohusiana na lile gari ni kuwa baada ya kuzungumza na wewe hii asubuhi, makao ya polisi wamenipigia simu na kunijulisha kuwa kumekuwa na tukio la kutatanisha nyumbani kwa waziri mkuu.” Mkuu wa kituo akaendelea kuniambia.
Aliponiambia hivyo nilishtuka sana. Nikajua arobaini zangu zimeshafika!
Je, nini kiliendelea? Usikose Ijumaa kwenye Gazeti la Ijumaa.