Enzi zetu ilikuwa raha sana, najua mtabisha maana mnajiona wajanja, lakini aise mmekosa mengi sana. Siku hizi shida tupu, nikikumbuka enzi zetu nawaonea huruma.
ule kwetu enzi zile ukitaka kuoa, unapeleka posa ikikubaliwa unapangiwa mahari, mara nyingi mahari ilikuwa ng’ombe wawili, mbuzi na kondoo mmoja, raha yake ilikuwa baba yako ndiye anayekulipia mahari.
Bibi harusi alikuwa hana gharama kabisa, akijitahidi kununua gauni lolote jeupe na kilemba cheupe, kamaliza vazi la harusi na bwana harusi hapo kuonesha unajali unajitahidi unamnunulia mchumba raba nyeupe, mchezo unakwisha hudaiwi kitu.
Siku ya harusi huna haja ya gari wala baiskeli, bibi harusi anatembea kwa mguu toka kwao mpaka kwako, mnaanza maisha, mambo simpo kabisa.
Ng’ombe walipoanza kuwa shida hasa kwa watu wa mjini, ndiyo ikaanza taratibu ya kulipa fedha badala ya wanyama kama mahari, ng’ombe alikuwa shilingi mia tano, mbuzi na kondoo shilingi thelathini.
Ukipangiwa mahari ya ng’ombe wawili na mbuzi wawili unalipa shilingi alfu moja na sitini, tena kwa kawaida mahari huwa haikamilishwi, hivyo ikikushinda kidogo hakuna kesi.
Sasa zama hizi kiboko, mtu unapangiwa mahari shilingi milioni mbili, halafu lazima utafute suti ya laki tano, magari ya kifahari, mipombe,
ukumbi, mivideo, kitu kama milioni kumi lazima zikutoke. Halafu kuna
hiki kichekesho kipya cha kuleta mizawadi kwenye ukumbi, vitanda
makabati mafriji, mafriza.
Vurugu tupu. Wiki moja baada ya harusi
maharusi wako hoi kifedha wanaanza kukopa hata hela ya kula. Acha
bwana enzi zetu ilikuwa raha sana.