
UONGOZI wa Polisi Tanzania umeridhishwa na kiwango cha mlinzi mkongwe, Kelvin Yondani na sasa unajiandaa kuendelea kumbakisha ndani ya klabu hiyo kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu Bara 2021/22.
Yondani alijiunga na Polisi Tanzania katika dirisha dogo la usajili na kusaini mkataba wa mwaka mmoja, ambapo mpaka sasa amesaliwa na miezi sita pekee ndani ya kikosi cha timu hiyo.
Julai 20, mwaka huu, Polisi ilitangaza kuachana rasmi na wachezaji wake 13, waliokuwa sehemu ya kikosi chao kwa msimu uliopita wa 2020/21.
Akizungumza na Championi Jumatatu, Ofisa Habari wa Polisi Tanzania, Hassan Juma alisema Yondani amekuwa na mchango mkubwa ndani ya klabu yao, na benchi la ufundi la klabu hiyo linahitaji kuona anaendelea kusalia ndani ya klabu hiyo.
“Mlinzi wetu Kelvin Yondani ataendelea kusalia ndani ya Polisi Tanzania kwa msimu ujao wa Ligi kuu Bara, hii ni kutokana na ukweli kwamba benchi letu la ufundi limeridhishwa na kiwango chake kwa kipindi cha nusu msimu alichokuwa nasi.
“Siwezi kuweka wazi ikiwa amesaini mkataba mpya au la, lakini kama klabu tupo kwenye mchakato wa kuhakikisha tunasuka upya tena kikosi chetu cha msimu ujao, kwa kuwapa mikataba mipya wachezaji waliosalia na kusajili wachezaji wapya.” alisema Juma.
JOEL THOMAS, Dar es Salaam