
KUPINDUA serikali iliyopo madarakani siyo jambo jepesi na mara nyingi majaribio ya aina hii, huwa yanakwama na pale yanapofanikiwa, huwa ni kwa msaada wa jeshi!
Hata hivyo, hali ni tofauti nchini Afghanistan ambapo wapiganaji wa Taleban, wamefanikiwa kuipindua serikali ya nchi hiyo baada ya kuuteka mji mkuu wa Kabul, ukiwa ni mji wa mwisho baada ya kuiteka miji yote mikubwa nchini humo.
Jumapili ya Agosti 15, wapiganaji hao walifanikiwa kuingia mpaka ikulu ya nchi hiyo, huku Rais Ashraf Ghani aliyekuwa madarakani, akitoroka saa chache kabla na kukimbilia Tashkent katika nchi jirani ya Uzbekistan huku duru nyingine za kiintelijensia zikieleza kwamba huenda amekimbilia Tajikistan akiwa njiani kuelekea nchini Urusi.
Hatimaye Taleban wamefanikiwa kuidhibiti Afghanistan, ikiwa ni miaka 20 tangu walipoondolewa madarakani kwa nguvu na kutamatisha karibu miaka 20 ya uwepo wa Marekani na washirika wake nchini humo.
Ukitazama jinsi mchakato mzima ulivyokuwa, kuanzia mwanzo mpaka mwisho, unaweza kufananisha na filamu ya kusisimua. Mji Mkuu wa Kabul umeingia kwenye machafuko, na wakazi na raia wa kigeni wamekuwa wakijaribu kutoroka kwa kupitia uwanja wa ndege wa mji huo, kabla haujadhibitiwa na wapiganaji hao.
Katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa mji mkuu huo, shuhuda mmoja ameliambia Shirika la Habari la BBC kwamba wafanyakazi wameacha madawati yao na watu wanakimbilia ndege katika hatua za kuokoa maisha yao.
Kabul ulikuwa mji mkuu wa mwisho nchini Afghanistan kudhibitiwa na Taliban huku kasi iliyotumika kukamata udhibiti huo ikiwashtua wengi.

Hatua hiyo imekuja wiki chache tu baada ya serikali ya Marekani ambayo kwa kipindi kirefu ndiyo iliyokuwa inaisaidia serikali ya nchi hiyo kubaki madarakani kwa ushirikiano wa majeshi mengine ya kigeni, kutangaza kuondoa vikosi vyake vyote nchini humo na kuiacha serikali ya nchi hiyo ijiendeshe yenyewe.
Rais wa Marekani Joe Biden ametetea kujiondoa kwa wanajeshi wa Marekani, akisema kuwa hakuweza kuhalalisha uwepo wa Marekani usio na mwisho katikati ya vita vya wenyewe kwa wenyewe vya nchi nyingine.
Zaidi ya nchi 60, pamoja na Marekani na Uingereza, zimetoa taarifa ya pamoja zikisema watu wa Afghanistan wanastahili kuishi kwa usalama na utu, na kwamba usalama na utawala wa kiraia unapaswa kurejeshwa mara moja.
Pia wametoa wito kwa Taliban kumruhusu mtu yeyote anayetaka kuondoka kufanya hivyo, na kuweka barabara, viwanja vya ndege na vivuko vya mipaka wazi.
Taliban waliwaamuru wapiganaji wao kuingia Kabul Jumapili, baada ya kuwazuia mapema nje kidogo ya jiji hilo na kueleza kuwa walikuwa wakienda kuzuia machafuko na uporaji baada ya vikosi vya usalama likiwemo jeshi la nchi hiyo, kuukimbia mji huo mkuu. Picha zilizotangazwa na mtandao wa televisheni wa Al Jazeera zimewaonesha wapiganaji hao wakiwa ndani ya ikulu ya rais wa nchi hiyo.
Kupitia ukurasa wake wa Mtandao wa Kijamii wa Facebook, Rais Ghani alisema kwamba aliamua kufanya uamuzi mgumu kuondoka ili kuepusha umwagaji damu katika mji mkuu huo.
Msemaji wa Taliban Suhail Shaheen ameliambia Shirika la Habari la BBC kuwa wananchi wa Kabul hawana haja ya kuwa na wasiwasi na kwamba mali na maisha yao yatakuwa salama chini ya usimamizi wa Taleban.
MAREKANI NA UINGEREZA ZATUMA VIKOSI KUWAONDOA RAIA WAKE
Marekani imepeleka maelfu ya wanajeshi kusaidia kuwaondoa wafanyakazi wake na Waafghan ambao walikuwa wakishirikiana nao katia kipindi chote walichokuwepo nchini humo.
Helikopta nyingi za kijeshi zinazosafirisha wafanyakazi wa ubalozi wa Marekani zilionekana katika anga la nchi hiyo Jumapili, na kulikuwa na ripoti za moshi unaofuka karibu na eneo la ubalozi wakati nyaraka muhimu zikiharibiwa na wafanyakazi wa ubalozi ili zisiangukie kwenye mikono ya wapiganaji hao.
Karibu wanajeshi 600 wa Uingereza wametumwa kusaidia operesheni yao ya kujiondoa na kuwaondoa wafanyakazi wote wa ubalozi wa nchi hiyo huku Waziri Mkuu wa Uingereza, Boris Johnson akisema kipaumbele chake ni kusaidia raia wa Uingereza na wote ambao walikuwa wakishirikiana nao kuhakikisha wanaondoka Afghanistan haraka iwezekanavyo.
Nchi nyingine pia zinawahamisha raia wao, na kupunguza uwepo wao nchini Afghanistan na wakati mwingine hufunga balozi zao kabisa. Urusi imepanga kuitisha mkutano wa dharura wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ili kujadili hali ya Afghanistan na kusema kuwa haitafunga ubalozi wake kwa sababu imepewa hakikisho la usalama na Taliban.