×

Waziri Alipokiri Kuwa Mchawi-27

ILIPOISHIA WIKIENDA
“Alfajiri ya leo gari hilo lilikutwa limeegeshwa sehemu likiwa halina mtu. Polisi wakalikamata. Tulipolipekua tulikuta likiwa na kadi iliyokuwa na jina lako. Kadi yenyewe ni hii hapa.”

Mkuu huyo wa kituo alinionesha kadi ya gari langu iliyokuwa juu ya meza yake.
SASA ENDELEA…

Nilipoitazama niligundua kweli ilikuwa kadi ya gari langu.
“Tukio la pili linalohusiana na lile gari ni kuwa baada ya kuzungumza na wewe hii asubuhi, makao makuu ya polisi wamenipigia simu na kunijulisha kuwa kumekuwa na tukio la kutatanisha nyumbani kwa waziri mkuu,” mkuu wa kituo akaendelea kuniambia.

Aliponiambia hivyo nilishtuka sana. Nikajua arobaini zangu zimeshafika!
Lakini nikaona ninyamaze tu na kumsikiliza, nikajidai kumuuliza:
“Tukio gani limetokea?”

“Kuna mtu ambaye alijipenyeza nyumbani kwa waziri mkuu jana usiku akiwa uchi wa mnyama na kwenda kujisaidia mbele ya mlango wa nyumba ya waziri mkuu.”
Wakati naelezwa hivyo nilikuwa nimemtumbulia macho mkuu wa kituo hicho.
Ili kujifanya si mimi niliyehusika na tukio hilo nikamuuliza:

“Huyo mtu aliingiaje nyumbani kwa waziri mkuu wakati kuna ulinzi?”
“Mpaka sasa haijafahamika lakini hakuingia kupitia kwenye geti na hakutoka kupitia kwenye geti. Polisi alimfuma wakati alipoingia ndani ya geti. Aliona mtu aliyekuwa uchi amechutama mbele ya mlango akijisaidia.

“Alipomuuliza alikuwa nani na anafanya nini yule mtu alisimama. Polisi huyo akarudi kwenye geti kuchukua silaha na kumuarifu mwenzake kuhusu mtu huyo na waliporudi tena hawakumkuta. Hawakujua ametokea kwa wapi.”

“Pengine alikuwa ni mwendawazimu,” nikajidai kumwambia mkuu huyo wa kituo ili kupoteza ile dhana ya uchawi.“Sasa swali tunalojiuliza aliingilia kwa wapi na alitokea kwa wapi?”

“Labda aliingilia hapohapo kwenye geti, wale polisi wanaweza kuwa walilala, hawakumuona.”

Jibu langu hilo likawa limemchanganya mkuu wa kituo hicho. Akaonekana kufikiri kidogo lakini hakutaka kukubaliana na mimi mara moja.
“Hilo haliwezekani. Wale polisi wanatakiwa kuwa macho wakati wote. Kama atalala ni mmoja tu mwenzake atakuwa macho.”

“Sasa unadhani nini kimetokea?”
“Bado tunaendelea na uchunguzi lakini kuna kitu kingine ambacho nilitaka kukueleza.”
“Kitu gani?”

“Ni kuhusu hili gari lako. Kuna jirani mmoja wa nyumba ya waziri mkuu amewaambia polisi kuwa lilikuwa limeegeshwa karibu na nyumba yake kwa muda mrefu jana usiku. Baadaye aliona mtu aliyekuwa uchi na mwenye wasiwasi akijipakia na kuondoka.

unashuku mtu huyo ndiye yule aliyeingia nyumbani kwa waziri mkuu.”
Hapo sikuwa hata na la kusema. Nikabaki kumtumbulia macho mkuu huyo wa kituo cha polisi.

“Bado tutasema kuwa huyo alikuwa mwendawazimu. Mwendawazimu anaendesha gari?”

“Unajua magari pia yanafanana, isijekuwa ameona gari jingine!”
“Tuko makini sana. Uchunguzi unaendelea wa kumtafuta yule mtu. Anatakiwa aeleze kwa nini alifanya kitendo kile nyumbani kwa waziri mkuu.”
“Ni kweli, lazima akamatwe ahojiwe.”

“Hatuna sababu ya kuendelea kulizuilia gari lako kwa sababu halikukamatwa katika eneo la tukio. Tutakukabidhi gari hilo kwa vile tunajua analo nani. Tutakapolihitaji tutalipata kwako.”
“Oh! Nashukuru sana.”

“Lakini kuna jambo moja tunalihitaji kutoka kwako.”
“Jambo gani?”
“Unatakiwa uandikishe kwamba gari lako liliibiwa usiku na utoe maelezo liliibiwa vipi.”
“Sawa nitafanya hivyo.”

Polisi huyo akainua mkono wa simu iliyokuwa juu ya meza yake, alibonyeza kiwambo cha simu ya ndani kwa ndani kisha akasema:
“Polisi mmoja aje ofisini kwangu.”
Akaurudisha ule mkono wa simu. Baada ya sekunde chache yule polisi aliyenileta mle ofisini aliingia.

“Nenda na mheshimiwa akaandikishe maelezo yake. Ukimaliza niambie nije nimkabidhi gari lake.”
“Sawa afande.”
Mkuu huyo wa kituo akanigeukia mimi.

“Sasa nenda na huyo askari, atakwenda kuandikisha maelezo yako halafu nitakuja kukukabidhi gari lako.”

Nikatoka na yule polisi. Tulikwenda kaunta ambako alitoa faili akaanza kuandikisha uongo wangu.
Baada ya kuandika jina langu, umri wangu na wadhifa wangu wa uwaziri, alitaka nimueleze jinsi gari hilo lilivyoibiwa.

Nilibuni tu jina la hoteli halafu nikamwambia:
“Nina kawaida ya kufika katika hoteli hiyo mara kwa mara pamoja na mke wangu.”

Leave a Comment