
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Ruangwa amechagua vijana saba kutoka kwenye mashindano ya kuwania kombe la Jimbo la Ruangwa ambapo Nkeng’ende FC iliichapa Mkangano FC 5-1 kwenye fainali na kuwa bingwa.
Katika mechi hiyo ya fainali iliyochezwa wikiendi iliyopita kwenye Uwanja Shule ya Awali Msingi ya Wonder Kids, Majaliwa alisoma majina hayo saba ya wachezaji ambao watajiunga na kambi ya timu ya vijana ya chini ya miaka 20 ya Namungo FC.
Waziri alisema, lengo la masindano hayo lilikuwa ni kuuibua vipaji kwa vijana ambao baadae wataichezea Namungo FC ya wilayani Ruangwa inayoshiriki Ligi Kuu Bara.
Mashindano ya kuwania kombe la Jimbo la Ruangwa yalishirikisha timu 32 kutoka Kata za jimbo hilo ambapo mshindi wa kwanza alipata kombe, kitita cha sh. milioni mbili, seti moja ya jezi na mpira.
Mshindi wa pili alijipatia shilingi milioni moja na nusu, seti moja ya jezi na mpira na mshindi wa tatu shilingi milioni moja, seti moja ya jezi na mpira.
ISSA LIPONDA, Dar es Salaam