
Rais Samia Suluhu Hassan amesema kuwa katika kipindi cha miezi 6 ambacho amekua Rais, kuna mengi amejifunza kutoka kwa viongozi mbalimbali ikiwemo Mawaziri ambao walikua wanamsoma na yeye akiwasoma.
Pamoja na hilo wapo baadhi ya Mawaziri ambao Rais amesema kuwa walichukulia hali ya ukimya wake kama udhaifu hivyo kuanza kufanya mambo wanavyojisikia wao.
“Katika kipindi cha miezi sita cha urais wangu nilijaribu kukaa kimya na kuwa mtulivu nikisoma kazi za wizara zote zinavyoendeshwa. Kuna mambo mengi ya kurekebisha, wakati ninawasoma Mawaziri, Manaibu, Makatibu wakuu na wao walikuwa wananisoma mimi.
“Wakati ninawasoma Mawaziri, Manaibu, Makatibu wakuu na wao walikuwa wananisoma mimi, wakachukulia ukimya wangu ni udhaifu, wakaanza kufanya yao yaliyowapendeza, lakini wengine walichukulia ukimya na utulivu wangu kama njia ya kuonyesha uwezo wao kufanya kazi.
“Nataka niwaambie kwamba kipindi cha miezi sita nilikuwa najifunza, kabla ya Urais nilikuwa Makamu wa Rais, nilikuwa na nyinyi nilishiriki mambo mengi lakini sikupata fursa ya ndani ya kujifunza. Nimejifunza na nimeona sasa jinsi gani nakwenda na nyie.
“Katika uongozi kuna mbinu nyingi, tumefundishwa staili nyingi, ipo ya carrot na ipo ya stick. Hivyo unaweza kutumia moja ama zote kwa pamoja. Mimi nimejichagulia njia yangu, tunakoendelea Serikali yetu itaendeshwa kwa matendo makali sio kwa maneno makali.
“Msinitegemee kwa maumbile yangu haya na malezi yangu nikae nianze kufoka hapa weye.. weye… wa.. wa.. wa.. Nahisi si heshima, kwa sababu nafanya kazi na watu wazima wanaojua jema na baya ni lipi, tunapozungumza tunaelewana kila mmoja anatimiza wajibu wake.
“Msitegemee nitafoka hovyo hovyo, kufokea watu wazima wenzangu, nitafoka kwa kalamu. Kwa kipindi cha miezi sita kuna watu walichukulia hii Serikali poa, Serikali cool, wakafanya wanayoyataka, leo nimeapisha mawaziri wanne na mwanasheria mmoja.
“Ninajua kuna wizara moja niliyoipangua ilipaswa iwepo uongozi wake uwepo hapa, uwape upya walioapishwa kwa sababu sio wizara ambayo waliapia nyuma. Hapa nilipofika nimeweka comma sio full stop, mabadiliko yanaendelea, tutaifanyia mabadiliko,” amesema Rais Samia.