
KOCHA mpya wa Simba Hitimana Thierry katika kukijenga kikosi hicho kuelekea katika michuano ya kimataifa ameweka wazi kuwa anahitaji timu ambayo kila mchezaji wa mbele atakuwa na uwezo wa kufunga mabao.
Thierry ambaye alijiunga na Simba hivi karibuni akitokea katika klabu ya Mtibwa Sugar.
Akizungumza na Championi Jumatatu, Hitimana alisema kuwa yeye kama kocha anaamini kuwa timu bora duniani ni ile ambayo kila mchezaji ana uwezo wa kufunga bao jambo ambalo linawafanya wapinzani wengi kushindwa kufahamu wachezaji wa kuwakaba.
“Timu bora na inayoogogwa katika ulimwengu wa michezo ni ile ambayo mpinzani hafahamu anaenda kumkaba nani uwanjani, kila mchezaji akiwa na uwezo wa kufunga na kutengeneza hatari kila wakati anaifanya timu hiyo kuwa tishio na ya kuogopwa.
“Natamani Simba iwe katika hali hiyo, nikiwa kama kocha kuanzia katika eneo la kiungo mpaka ushambuliaji natamani kuona wachezaji wote wanakuwa tishio na wenye kuleta madhara kwa wapinzani.
“Hata ukiitazama michuano ya kimataifa utaona ni jinsi gani timu ambazo zinafanya vizuri ni zile ambazo zina wachezaji wengi kuanzia eneo la kiungo mpaka ushambuliaji wenye madhara wakiwa na uwezo wa kufunga magoli na kutengeneza pia,”alisema kocha huyo.
MARCO MZUMBE, Dar es Salaam