Idadi ya watu waliokufa nchini Sierra Leone baada ya lori la kubeba mafuta kulipuka imefikia watu 99. Ajali hiyo ilitokea katikati ya mji mkuu wa taifa hilo, Freetown
Naibu waziri wa Afya wa Sierra Leone, Amara Jambai amesema kufikia sasa watu 99 wamefariki dunia kutokana na mlipuko wa lori la mafuta uliotokea katika mji mkuu, Freetown
Picha na mikanda ya video inayosambaa kupitia mitandao ya kijamii imeonesha watu walioungua vibaya wakiwa wamelala kwenye mitaa ya mji wa Freetown huku moto ukiteketeza pia maduka na nyumba zilizo karibu.

Mlipuko huo ulitokea jana Ijumaa baada ya lori la mafuta kugongana na basi katika kitongoji cha Wellington mashariki mwa mji mkuu, Freetown.
Miongoni mwa waliofikwa na mkasa huo ni wale waliokimbilia kuchota mafuta. Kwa mujibu wa mmoja wa wauguzi katika moja ya hospitali walikofikishwa waathiriwa wa mlipuko huo, kati ya watu aliowahudumia ni pamoja na wanawake, wanaume na watoto, waliojeruhiwa vibaya.

Rais wa Sierra Leone Julius Maada Bio aliyeko nchini Scotland akihudhuria mkutano wa Umoja wa Mataifa wa mabadiliko ya tabia nchi kupitia ukurasa wake wa twitter, ametuma salamu za rambirambi kwa familia zilizowapoteza wapendwa wao kwenye ajali hiyo na waliojeruhiwa na kuongeza kuwa, amesikitishwa na mkasa huo wa kutisha uliogharimu maisha ya watu.
Amesema, serikali yake itafanya kila juhudi kuhakikisha familia zilizoathirika kutokana na ajali hiyo zinapatiwa msaada.
Meya wa mji wa Freetown, Yvonne Aki-Sawyerr amesema madhara na hasara kamili ya ajali hiyo bado haijajulikana lakini polisi na maafisa wengine wa serikali wako eneo la tukio kutoa msaada unaohitajika.
