
WAZIRI wa Mambo ya Ndani wa Kenya, Fred Matiang’i amezungumzia kuhusu zawadi ambayo serikali ilikuwa imeahidi kutoa zaidi ya kiasi cha Tsh bilioni 1.23 kwa atakayetoa taarifa za watuhumiwa wa ugaidi waliotoroka gerezani.
Wananchi wamekua wakishinikiza kutaka waliohusika katika kusaidia kukamatwa kwa washukiwa watatu wa ugaidi kupewa KSh 60M ambazo DCI waliahidi. Waziri Matiang’i hata hivyo amesema hilo si muhimu kwa sasa na hakudhibitisha iwapo zawadi itatolewa.
Kitita hicho kilikuwa cha kwa atakayetoa taarifa kuhusu washukiwa wa ugaidi waliotoroka gerezani huko Kamiti. Musharaf Abdalla, Mohamed Ali Abikar na Joseph Juma Odhiambo walikamatwa katika eneo la Malalani Endau Kitui baada ya umma kutoa taarifa kuwahusu.
Mtu aliyehusika katika kuwakamata watatu hao amesema walitambua hawana silaha na ndipo wakafaulu kuwakamata.
Waziri Matiangi ambaye alikuwa amefika Kamiti kushuhudia kurejeshwa kwa wafungwa hao hata hivyo alidinda kudhibitisha iwapo serikali itatekeleza ahadi yake. Mwanahabari waCitizen TV, Hassan Mugambi ndiye aliyemuuliza Matiangi iwapo sasa waliowajulisha polisi kuhusu washukiwa hao watazawadiwa.
“No…no…no, hatutaenda hiyo njia kwa sasa. Wacheni tusianze kushuku lolote wakati huu. Tutashughulikia hili kwa umakini mkubwa kama wenzangu walivyosema,” Matiang’i alisema.
Wakenya ambao wamekuwa wakifuatilia habari kuhusu wahalifu hao kwa kina walitaka ahadi ya zawadi hiyo ya KSh 60M kutimizwa. Kupitia mtandao wa twitter, Wakenya waliitaka serikali kuhakikisha kuwa inawapa waliohusika kitita hicho.
Hata hivyo, baada ya jibu la Matiang’i huenda ikawa ngumu kwa waliohusika kupokea mkoba huo kutoka kwa serikali. Watuhumiwa hao walikuwa katika eneo la Malalni. Muuzaji katika duka moja aliwatambua watatu hao na kuwajulisha wenzake lakini wakahofia kuwakamata wakihofia wamejihami.
Walikuwa wamefika hapo kununua maziwa, maji na biskuti ikishukiwa njaa iliwakata maini walipokuwa wamejificha katika msitu wa Mwingi Game Reserve.
Mkuu wa Polisi Kitui, Leah Kithei alisema watatu hao walikamatwa katika eneo la Mwingemi wakijaribu kuingia barabara ya Mwingi-Garissa. Watatu hao wanatambuliwa kama Musharaf Abdalla Akhulunga almaarufu Shukri, Mohamed Ali Abikar na Joseph Juma Adhiambo almaarufu Yusuf.