×

Familia: Rayvanny Anaoa Wote Paula, Fahyma

KUFUATIA mgagaziko juu ya ni nani atakuja kuwa mke halali wa staa mkubwa wa Bongo Fleva, Raymond Shaban Mwakyusa almaarufu Rayvanny kati ya Paula Kajala na Fahyma, hatimaye familia kupitia kwa kaka yake imevunja ukimya kuhusu suala hilo.

NZOVWE, MBEYA

Gazeti la IJUMAA limefunga safari kutoka katika ofisi zake zilizopo Sinza-Mori jijini Dar hadi jijini Mbeya maeneo ya Nzovwe ambako ndipo nyumbani kwa wazazi wa Rayvanny au Chui kwa lengo la kufanya mahojiano kamili na familia hiyo.

IJUMAA limefanikiwa kuwakuta baadhi ya ndugu zake ambapo mazungumzo yalikuwa hivi;

IJUMAA: Hodi mpaka ndani…

KAKA WA RAYVANNY: Karibu… karibu.

IJUMAA: Nashukuru sana, mimi ni Mwandishi wa Gazeti la IJUMAA, ninahitaji kuzungumza na mama yake Rayvanny, je, nimemkuta?

KAKA WA RAYVANNY: Kwa bahati mbaya hujamkuta, mama amesafiri, ni muda sasa hayupo nyumbani.

IJUMAA: Ooo! Unaweza kuniambia amekwenda wapi na wewe na Rayvanny mko vipi?

KAKA WA RAYVANNY: Mama amekwenda kijijini Tukuyu na mimi ndiye kaka mkubwa wa Ray (Rayvanny).

IJUMAA: Ni kweli mnafanana sana, lengo la kuja hapa ni kutaka kuzungumza na mama kuhusu ishu ya warembo wawili, Paula na Fahyma ambao wote wametoka kimapenzi na Rayvanny, kuna sintofahamu ambayo inaendelea mitandaoni ambapo kuna baadhi ya watu wanadai staa huyo hivi karibuni atafunga ndoa na Paula na wengine wanadai haiwezekani, labda afunge na Fahyma kwa kuwa tayari ameshazaa naye, ninyi kama familia, mnalionaje hilo?

KAKA WA RAYVANNY: (anacheka) kwani mwanaume akishazaa na mwanamke ndiyo lazima amuoe?

IJUMAA: Lakini wametoka mbali…

KAKA WA RAYVANNY: Sawa, ila kuna watu wamezaa hadi watoto watano huko nje na bado hawajawaoa hao wanawake waliozaa nao.

IJUMAA: Kwa hiyo unataka kumaanisha kwamba hapa Fahyma hana chake?

KAKA WA RAYVANNY: Hapana, sijamaanisha hivyo, hayo umeongea wewe siyo mimi.

IJUMAA: Ni kweli kwamba Rayvanny na Fahyma wamewahi kufunga ndoa ya kimila?

KAKA WA RAYVANNY: Hayo ni mambo yao binafsi sana, nadhani anatakiwa awahakikishie yeye mwenyewe; yaani Rayvanny.

IJUMAA: Kwa upande wako kati ya Paula na Fahyma, unatamani nani aolewe na mdogo wako?

KAKA WA RAYVANNY: Mimi siwezi kumchagulia mwanamke wa kuoa kwa sababu hata kwangu hakufanya hivyo, lakini binafsi naona siyo mbaya kama anawaoa wote wawili (Paula na Fahyma).

IJUMAA: Kwa nini unasema awaoe wote wawili wakati yeye ni Mkristo na tunajua dini haimruhusu?

KAKA WA RAYVANNY: (anatabasamu) aliyekuambia Rayvanny ni Mkristo ni nani?

IJUMAA: Hee! Makubwa mbona kipindi chote watu ndiyo wanajua hivyo na majina yake yanafahamika kama Raymond Mwakyusa?

KAKA WA RAYVANNY: Ooh kumbe! Sasa hilo jina la Shabani pale katikati linatafuta nini?

IJUMAA: Ina maana anaitwa Raymond Shabani Mwakyusa?

KAKA WA RAYVANNY: No comment.

IJUMAA: Kwa hiyo Paula huwa anawasiliana na mamamkwe wake mara kwa mara? Maana sasa hivi Fahyma na Rayvanny wameshaachana?

KAKA WA RAYVANNY: Aliyewaambia Fahyma na Rayvanny wameachana ni nani? Watu wanaongea mambo ambayo hawana uhakika nayo kabisa.

IJUMAA: Mmm! Sasa kama hawajaachana, basi Fahyma atakuwa na moyo wa uvumilivu sana.

KAKA WA RAYVANNY: Kwa nini?

IJUMAA: Kwa sababu mwanamke anayejielewa, hawezi kuruhusu mwanaume wake aposti picha za kimahaba akiwa na mwanamke mwingine halafu anyamaze tu.

KAKA WA RAYVANNY: Kwani kumposti mtu ni dhambi? Rayvanny ni msanii mkubwa hivyo ana uwezo wa kumposti mwanamke yeyote yule na kusiwe na tatizo lolote.

IJUMAA: Kuna baadhi ya watu wanadai kuwa Rayvanny ni msanii mkubwa, lakini ameshindwa kumfungulia biashara nzuri mama yake na badala yake anaishia kufanya biashara ndogondogo sokoni, wewe hili unaliongeleaje?

KAKA WA RAYVANNY: Watu kila siku wanaongea tu na huwezi kuwazuia kusema, ni kweli Rayvanny ni msanii mkubwa na ana pesa, lakini haimaanishi kwamba yeye ndiye awajibike kwa kila kitu huku nyumbani.

Jambo lingine hata kama ana pesa atahudumia watu wangapi? Maana ana ndugu wengi sana, akisema amhudumie kila mtu, hataweza.

IJUMAA: Lakini yule ni mama yake, ilitakiwa ampe kipaumbele katika matunzo.

KAKA WA RAYVANNY: Kuna vitu vingine mtu huwezi kuvibadilisha, pengine mama mwenyewe anapenda au hayo maneno ya kwamba anauza mboga sokoni huwenda yakawa siyo ya kweli maana kila mtu huwa anaongea lake siku hizi.

IJUMAA: Asante sana kwa muda wako.

KAKA WA RAYVANNY: Karibu sana.

STORI: MEMORISE RICHARD, MBEYA

Leave a Comment