
MBUNGE wa kuteuliwa, Humphrey Polepole amesema kuna baadhi ya watu ndani ya Serikali (ambao hajawataja) wamekuwa wakifanya vitu vya hovyo kuifanya Serikali ambao amedai wamekuwa ni kwa masilahi yao binafsi na si kwa ajili ya Taifa.
Polepole amesema hayo leo Jumamosi, Desemba 11, 2021 wakati akizungumza na wanahabari katika Ukumbi wa LRHC, Kijitonyama, Dar es Salaam.
“Kama viongozi wasiposali na kumtemea Mungu nchi yetu haiwezi kuendelea, tumtangulize Mungu mbele. Kuanzia diwani, mpaka mawaziri na kule juu tuwe watu wa maombi, kukumbushana ni muhimu, naona kama tunatakiwa tuishi maisha ya Kimungu hivi. Viongozi wanatakiwa wawe waadilifu na wanyenyekevu.
“Kwenye mgongano wa kimasilahi kuna aina tatu, masilahi ya Taifa, kundi au mtu mmoja mmoja, wanaanza na masilani ya mtu mmoja, kisha kundi na baadaye Taifa, nikasema wanaopanga hivi ni wahuni.
“Wahuni wanapenda masilahi binafsi kwanza, kazi yetu ni kuwadhibiti bila huruma wala kucheka nao. Yanatokea majitu tena viongozi na kusema mimi ni muhuni nimepenya, unaweza kutafakari namna gani kiongozi huyu yuko serious, huwezi kuwa kiongozi ukachekelea kuwa mhuni.
“Kule bungeni tunakutana mara chache, mfano kuna kipindi cha mwezi Machi hadi Julai, ina maana mimi niongee mara nne tu kwa mwaka kuhusu wahuni, unadhani inatosha, nitatumia fursa zozote za kusema ili kuwasema wahuni.
“Kwa sasa nimeshaanza kufuatilia mambo kadhaa, watu wakizingua pahala ninatoka ninasema hapa umezingua nitaruka na wewe, nakulipua, si wanachelewa kuchukua hatua?
“Nilisema kuhusu magonjwa, mfano ebola, kesi moja tu imewahi kupenya na ikafuatiliwa na sasa tuko salama. Yakaja haya magonjwa mengine maarufu hivi karibuni lakini sio kitu. Nikasema muwe makini hawa wahuni wa kimataifa ni wajanja.
“Nilieleza kuhusu uchambuzi wa matatizo, malaria haiishi Tanzania kwa sababu hatuchambui tatizo, unadhani ufumbuzi ni chandarua kwani ukitoka usiku kwenda haja ndogo mbu si wanaunga na wewe? tunafanya maamuzi ambayo hayajajengwa katika kutatua tatizo, hilo nalo tatizo.
“Kuna kiwanda kipo hapa nchini kinatengeneza viuatilifu vya kuua mazalia ya mbu, nyie wanahabari waulizeni wamewahi kunnuua pale? Mtu analala kwenye chandarua mguu upo nje, mbu wanamng’ata, nauliza sisi tumekwenda shule tukasoma, hii ndio suluhisho kweli?” amesema Polepole.