×

Sakata la Machinga, Polepole Ahoji “Mhe. Rais Aliwatuma Hivyo?”

MBUNGE wa kuteuliwa, Humphrey Polepole amewataka viongozi wanaosimamia mamlaka za miji na majiji kuhakikisha wanafuata maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan kuhusu kuwapanga wamachinga badala ya kutumia nguvu kuwaondoa bila utaratibu wala kutojua wanawapeleka wapi.

 

Polepole amesema hayo leo Jumamosi, Desemba 11, 2021 wakati akizungumza na wanahabari katika Ukumbi wa LRHC, Kijitonyama, Dar es Salaam.

 

“Nilizungumza kuhusu songombingo la wamachinga, Mhe. Rais Samia Suluhu alitoa maelekezo mazuri sana lakini wapo waliotekeleza vizuri wengine wamefanya vibaya mno, wameboronga, ukimkosoa DC au RC kuhusu hili wanasema umemkosoa Rais, nani kakwambia?”

 

“Rais Samia Suluhu alitoa maelekezo mazuri sana kuhusu wamachinga, wapangeni vizuri, msiwazonge, msiwapige, msiwanyanyase…. mimi ni mwana-CCM bana, fitina kwangu ni mwiko. Nikasema mlivyotenda kwa machinga baadhi yenu mmekosea na nikatoa mifano.”

 

“Suala la machinga wanasema nimesema uongo, tena kwenye hilo nitasema na mengine ambayo sikutaka kusema, nina ushahidi, nimepeleka watafiti wilaya zote za Dar es Salaam, mtu amehamishwa na kupelekwa kwenye karo la choo, hivi Mhe. Rais aliwatuma hivyo?” amesema Polepole.

Leave a Comment