×

Pluijm afichua kilichomleta Nonga Yanga

pluijmMholanzi, Hans van Der Pluijm.

Hans Mloli, Dar es Salaam
WAKATI wengi wakijiuliza wingi wa mastraika kwenye kikosi cha Yanga baada ya kutua kwa Paul Nonga, bosi wa benchi la ufundi la timu hiyo, Mholanzi, Hans van Der Pluijm, amefichua kilichopo nyuma ya pazia kwamba kwa nini amemvuta mshambuliaji huyo kundini.

Nonga aliyewahi kuitumikia Mbeya City, ametua Yanga akitokea Mwadui FC kwa kusaini mkataba wa miaka mwili na kuongeza idadi ya washambuliaji wa kati wa timu hiyo kuwa watano, wengine ni Malimi Busungu, Matheo Simon, Mrundi, Amissi Tambwe na Mzimbabwe, Donald Ngoma.

Pluijm ameliambia Championi Jumatatu kuwa, amemteua Nonga kutua hapo kwa kuwa alihitaji straika mpambanaji, mjanja, anayelijua lango na mwepesi, kwamba hata ikitokea hitilafu ya mastraika alionao sasa, asikune kichwa katika kuziba pengo na mambo yaende kama hakuna tatizo.

“Bado Nonga hajaanza mazoezi na timu, natarajia Jumatatu (kesho) ataanza rasmi kwa ajili ya kujiandaa na michezo mingine, idadi ya mastraika imekuwa kubwa lakini (Nonga) amekuja hapa kuongeza changamoto na kuleta tija.

“Kuna michuano mingi na huwezi kujua nini kitatokea mbele, unaweza kupata majeruhi halafu ikashindikana la kufanya lakini unapokuwa na mtu kama Nonga, hakuna tatizo maana ataziba pale kwenye shida na tutasonga mbele ingawa juhudi zake zaidi zitachangia kuzidi kumuamini,” alisema Pluijm.

Leave a Comment