Hans Mloli, Dar es Salaam
KADIRI siku zinavyozidi kusonga, Yanga inazidi kudhihirisha kuwa haikukosea kuwasajili Wazimbabwe, Thabani Kamusoko na Donald Ngoma kutokana na maajabu wanayoendelea kuyafanya kwenye kikosi hicho.
Wachezaji hao wameuthibitisha zaidi ubora wao katika mechi mbili za mwisho za timu hiyo kwa kuchangia kwa asilimia 100 ushindi wa timu hiyo na kukusanya jumla ya pointi sita zilizowaweka kileleni kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara.
Katika mechi yao ya African Sports waliyocheza Tanga, timu hiyo ilishinda kwa bao 1-0 lakini juhudi binafsi za wachezaji hao ndizo zilikuwa chachu ya ushindi huo kwenye dakika ya 90 baada ya Ngoma kutoa pasi ya mwisho kabla ya Kamusoko kupiga shuti na kuibua matumaini.
Kama hiyo haitoshi, katika mchezo wao wa juzi dhidi ya Stand United, licha ya Kamusoko kukamata sehemu ya kiungo na Ngoma kusumbua vilivyo ukuta wa Stand, walichangia mabao matatu kati ya manne yaliyofungwa na
timu hiyo.
Bao la kwanza alifunga Mrundi, Amissi Tambwe ikiwa baada ya kupokea pasi ya mwisho maridadi ndani ya eneo la hatari kutoka kwa Kamusoko ambaye pia alikuwa na uwezo wa kufunga, bao la pili lilifungwa tena na Tambwe baada ya kuunganisha krosi safi ya Juma Abdul.
Bao la tatu ambalo liliwakuna mashabiki wengi, alifunga tena Tambwe kwa shuti kali nje ya 18 kwa kutengewa mpira kwa pasi ya mwisho ya Ngoma kabla ya Kamusoko kupiga kichwa safi na kuifungia Yanga hesabu ya mabao siku hiyo.
Kwa matokeo hayo, mpaka sasa Tambwe amefunga mabao nane sawa na Ngoma, ikiwa ni tofauti ya bao moja dhidi ya kinara Elias Maguri wa Stand United aliyeganda na mabao yake tisa aliyoyapata kabla ya mapumziko marefu ya ligi.
Ishu nyingine ni kwamba Yanga ina mabao 27 ambayo ni mengi zaidi ya timu nyingine zote, lakini katika kuonyesha umuhimu wa usajili wa Wazimbabwe hao pamoja na Tambwe, wamechangia mabao 19 kwa maana ya Tambwe na Ngoma nane kila mmoja, Kamusoko matatu na mengine nane yaliyosalia yakifungwa na wachezaji wengine.
Kuhusiana na hilo, Kamusoko amesema: “Nafurahi kuona hivyo lakini pongezi ni kwa timu nzima, nikiwa peke yangu siwezi kuwepo kila mahali uwanjani na kupata matokeo, bila wenzangu nisingefika hapa nilipo.”
