×

TGNP Yatoa Mafunzo ya Bajeti ya Mrengo wa Kijinsia Manispaa ya Kinondoni

Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Shedrack Maximmilian (kulia) akifungua mafunzo hayo. Kushoto ni Mjumbe wa Bodi ya TGNP Bi. Jovita Mlay.

 

 

 

MTANDAO wa Kijinsia nchini (TGNP) umetoa mafunzo ya bajeti yenye mrengo wa kijinsia kwa wakuu wa idara katika Manispaa ya Kinondoni, Dar es Salaam na kueleza umuhimu wa mafunzo hayo katika jamii ya kisasa.

 

Mafunzo hayo yalifunguliwa na Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Shedrack Maximmilian na kutolewa na Mjumbe wa Bodi ya TGNP, Bi. Jovita Mlay.

Bi. Jovita Mlay akitoa somo kwa washiriki.

 

 

 

Idara zilizopewa mafunzo hayo ni idara za Utawala na Utumishi, Fedha na Biashara, Afya na Kinga, Kilimo na Ushirika, Mifugo na Uvuvi, Elimu ya Msingi, Elimu ya Sekondari, Maendeleo ya Jamii na Vijana, Idara ya Mipango Takwimu na Ufuatiliaji, Idara ya Uhandisi, na Idara ya Mipango Miji na Mazingira.

 

Akielezea changamoto mbalimbali zinazotokana na tofauti za kijinsia Bi. Jovita alisema wamama wamekuwa wakiishi kimateso kutokana na mfumo wa maisha uliopo na wengi kuonekana masokoni wakifanyabiashara huku wakiwa na watoto migongoni na pengine wamewalaza kando ya barabara wakipigwa vumbi na kuhatarisha usalama wao kwa ajali za barabarani.

Mafunzo yakiendelea.

 

 

 

Bi. Jovita alitoa wazo kwa serikali kuanzisha vituo vya malezi ya watoto sehemu za kazi ili kumpunguzia mwanamke ugumu wa kazi anaokumbana nao kwenye kujenga taifa.

 

Akiendelea kutoa mifano inayomgandamiza mwanamke, Bi. Jovita amesema siku moja akiwa Longido mkoani Arusha amewahi kukutana na mama mjane na binti yake wakichunga mifugo na alipojaribu kuwaambia wamuuzie mbuzi mmoja walimwambia asubiri mpaka wakapate ruhusa kwa mtoto wa kiume ambaye ndiye mdogo kuliko wote lakini kwakuwa yeye ni mwanaume hivyo kiutamaduni wao ndiye mwenye maamuzi katika masuala ya kifamilia.

Washiriki wakiendelea kupata mafunzo.

 

 

 

“MWANAUME NI KICHWA”

Akiendelea kutoa somo Bi. Jovita aliiomba jamii kuachana na kauli zilizopitwa na wakati kama kauli maarufu isemayo mwanaume ni kichwa, kauli ambayo dhana yake kubwa ni kumgandamiza mwanamke.

 

KURUDISHWA MASHULENI WANAFUNZI WALIOZALISHWA

Akizungumzia suala ya kurudishwa shuleni wanafunzi waliopewa ujauzito na kujifungua Bi. Jovita amesema katika mchakato huo ni lazima mambo kadhaa yazingatiwe na kusema;

 

“Kwanza ni lazima yatengenezwe mazingira bora kwa huyu mwanafunzi, walimu nao waandaliwe kwa ajili ya kumpa elimu stahiki mwanafunzi huyo, watoto wao nao waandaliwe mazingira bora ili mzazi aweze kusoma kiutulivu, hivyo serikali inapopanga bajeti ni muhimu kuangalia mrengo wa kijinsia ili kumpa elimu stahiki mwanafunzi huyu,” alisema Bi. Jovita.

Washiriki wakifanya mpango kazi kwa kushirikiana baada ya mafunzo hayo.

 

 

 

VIKUNDI VYA WAMAMA VIELIMISHWE NAO WAELIMISHE WENZAO JUU YA MFUMO DUME

Bi. Jovita akitoa somo alisema kuna umuhimu mkubwa wa kutoa elimu kwenye vikundi vya kinamama ili nao watoe elimu kwa wenzao juu ya kupambana na mfumo dume kwenye jamii.

Picha ya pamoja baada ya mafunzo hayo kutoka kushoto waliokaa ni Afisa wa TGNP, Hellen Urio, katikati Bi. Jovita Mlay na wengine ni washiriki wa mafunzo hayo.

 

 

 

ELIMU YA KIJINSIA ITOLEWE KWENYE NYUMBA ZA IBADA

Baada ya mafunzo hayo washiriki nao walipata nafasi ya kuuliza maswali ili kuelewa zaidi na wengine kutoa ushauri wao katika kuboresha mafunzo hayo ambapo mmoja wa washiriki aliiomba TGNP kushirikiana taasisi za kidini kama vile makanisa na misikiti kutoa elimu ya kuondokana na mfumo dume na kuchukulia mambo kwa mrengo wa kijinsia.                                                            HABARI/PICHA ZOTE NA RICHARD BUKOS/ GPL

Leave a Comment