
JINA la mshambuliaji wa Mkongomani, Fabrice Ngoma anayekipiga Klabu ya Raja Casablanca ya nchini Morocco limeingia kwenye orodha ya washambuliaji wanaowaniwa na Yanga.
Hiyo ni katika kuelekea usajili wa dirisha dogo ambalo tayari limefunguliwa tangu juzi Jumatano kwa timu kushiriki kuviimarisha vikosi vyao.
Mshambuliaji wa Orlando Pirates anayekipiga kwa mkopo As Vita, Jean-Marc Makusu Mundele naye ni kati ya washambuliaji wanaotajwa kusajiliwa na timu hiyo katika dirisha dogo.
Mmoja wa mabosi wa Yanga, ameliambia Championi Ijumaa kuwa, majina hayo mawili ndiyo yaliyokuwepo mezani katika Kamati ya Mashindano ya timu hiyo, inayoongozwa na mwenyekiti wake, Rogers Gumbo.
Bosi huyo alisema kuwa, kati ya washambuliaji hao wawili kutoka DR Congo mmoja ndiye atakayesajili katika dirisha katika kuiboresha safu yao ya ushambuliaji inayoongozwa hivi sasa ni Fiston Mayele na Heritier Makambo.
Aliongeza kuwa kamati hiyo imepanga kusajili winga mmoja mwingine mwenye uwezo wa kufunga na kutengeneza nafasi za mabao.
“Tumepanga kufanya usajili mkubwa katika usajili wa dirisha dogo na kati ya hao tutasajili winga na mshambuliaji mmoja mwenye uwezo mkubwa wa kufunga.
“Awali lilikuwepo jina moja pekee la Makusu, lakini hivi sasa limeongezeka moja ambalo ni Ngoma ambaye pia
kutoka DR Congo.
“Uongozi umeanza kufanya naye kwa ajili ya kumsajili katika usajili huu wa dirisha uliofunguliwa jana (Jumatano), hivyo kama wakifikia muafaka mzuri basi atasajiliwa.
“Majina ya washambuliaji hayo yote mikononi mwa Nabi ambaye yeye ataamua mshambuliaji mmoja asajiliwe kati ya hao,” alisema bosi huyo.
Mjumbe wa Kamati ya Mashindano wa Yanga, Injinia Hersi hivi karibuni alizungumzia usajili na kusema kuwa:
“Tumepokea ripoti ya kocha wetu Nabi ikiagiza kusajili mshambuliaji na winga pekee, hivyo muda wowote
tutakamilisha mahitaji yake kwa kusajili wachezaji hao. Uongozi tunaahidi kufanya usajili mkubwa.”
WILBERT MOLANDI NA MUSA MATEJA