ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA:
Tulipofika polisi tulikwenda moja kwa moja kwa Inspekta Ben Matwanga na tuliambiwa yupo na kwamba alikuwa na mahojiano na yule mwanamke aliyemfanya zezeta kaka yangu.SONGA NAYO…
Tuligonga mlango wa ofisi ya mkuu huyo wa polisi akaturuhusu kuingia. Tulipoingia tulionana ana kwa ana na mwanamke huyo ambaye aliinamisha kichwa chake kwa aibu.
“Karibuni. Huyu mama amekiri kuwafanya mazezeta wale watu,” alisema Kamanda Matwanga.“Sasa mtafanyaje? Hana dawa za kuwarejeshea akili zao?”
“Amesema anaweza kujaribu…”
“Kujaribu? Kama anayo hiyo dawa ni bora akaenda kuwarudishia hali yao ya kawaida,” nilimkatiza kamanda ambaye alimgeukia yule mwanamke.
“Sasa mama itabidi twende nyumbani kwako ukachukue ile dawa kisha ukawape wewe kule hospitali ili wapone.”
“Lakini afande mambo hayo ya ndumba yataruhusiwa hospitali?” aliuliza yule mwanamke.“Ukiwa na sisi hakuna kitakachoshindikana.”
Tuliondoka kituoni, mimi, polisi watatu, wawili walikuwa vijana waliokuwa na bunduki na Kamanda Matwanga. Gari liliwasha taa na king’ora ili magari mengine yatupishe. Safari ikaanza.
Tulipofika nyumbani kwa mwanamke huyo tuliingia ndani akachukua dawa iliyokuwa kwenye chupa. Kama ilivyo ada, wakati tunatoka tayari watu walikuwa wamejazana kwenye geti ili kuona kitakachoendelea. Nadhani walidhani kuna misukule wengine tumekuja kuwachukua.
Gari hilo la polisi lilienda moja kwa moja hospitali.
“Mimi ni kamanda wa upelelezi wa wilaya,” alijitambulisha Inspekta Ben Mtwanga kwa wauguzi waliokuwa mapokezi.
“Tukusaidie nini?”
“Tunataka kuwaona wale wagonjwa tuliowaleta hapa ambao ni mazezeta.”
“Nisubirini kidogo nikamuone dokta,” akasema nesi mmoja.
Alikwenda kwenye ofisi ya bosi wao na akatoka naye, kumbe ni Dokta Namahonga.
“Ahaa, mmerudi tena. Nimeambiwa kuwa afande unataka kuwaona wagonjwa wale mliowaleta.”
“Sawa kabisa. Nikathibitishe mambo fulani ya kipolisi.”
“Hakuna tatizo, wapeleke wakawaone,” alisema Daktari Namahonga.
Tulikwenda mimi, yule mwanamke aliyewafanya mazezeta wagonjwa wetu, Kamanda Matwanga na wale askari wawili wenye silaha hadi kitandani kwa wagonjwa.
Alichokifanya ni kuwanusisha ile chupa yenye dawa wale wagonjwa. Alifanya hivyo mara tatu kisha wote wakapiga chafya.
“Tayari,” alisema yule mwanamke, sisi tukaduwaa.
“Ina maana kazi imekwisha?” aliuliza Inspekta Matwanga.
“Ndiyo,” akajibu, akaongeza: “Baada ya dakika kumi watakuwa wamerejesha akili.”
Tulikaa kwa dakika kumi na kweli kaka aliniangalia na kuniita kwa sauti ya kinyonge, “ Jerome.”
Niliinama pale kitandani na kumkumbatia. “Kaka, umepona!”
Nilianza kutokwa na machozi naye pia akawa analia. Yule mgonjwa mwenzake naye akawa anashangaa kinachoendelea baada ya kurejea fahamu zake.
Wodi hiyo ilikuwa ni ya wagonjwa wenye matatizo ya akili lakini baada ya kaka na yule mwenzake Banda kurejea katika hali ya kawaida aliitwa Dk. Namahonga ambaye baada ya kuwaona alishangazwa na tukio hilo. Aliwauliza wagonjwa maswali mbalimbali na wakawa wanajibu kiufasaha kabisa.
“Wahamishie wodi ya kawaida,” aliamuru Dk. Namahonga.
* * *
Baada ya wiki mbili kaka yangu Edgar na mgonjwa mwenzake Banda wakawa wamepona kabisa na yule mwanamke aliyewafanya zezeta alikuwa amekwishapelekwa mahakamani mara kadhaa na sisi, yaani mimi, kaka Ipacho na Bwana Makang’ako tuliitwa kutoa ushaidi.
Siku ya hukumu wote sisi tulikuwa katika Mahakama ya Wilaya ya Lilongwe ambapo yule mwanamke alikuwa kizimbani akisubiri hukumu kwa kosa lake la kuwatesa wanadamu kwa kuwaharibu akili na hasa baada ya kukiri kufanya kosa hilo alipoulizwa sababu alisema:
“Hakuna sababu nyingine isipokuwa yalikuwa ni masharti ya mganga wangu. Aliniambia lazima niwe na watu kama hawa ili biashara zangu zisonge mbele nizidi kutajirika.”
Baada ya kusema hayo ukumbi mzima ulizizima kwa kuguna, “Mhhhhh!”
“Kutokana na kukiri ulichokifanya mahakama hii inakufunga kifungo cha miaka kumi jela ili iwe fundisho kwa wengine wenye kufanya au wanaotaka kutenda vitendo kama hivyo. Unaruhusiwa kukata rufaa,” alisema Hakimu Noel Sinyaapi na kusimama kisha kuinamisha kichwa na akatoweka kuelekea kwenye ofisi yake.
Mwanamke huyo mkatili alifungwa pingu na kupelekwa gerezani.
Tulipotoka mahakamani wote tulikwenda kwa Bwana Makang’ako kusherehekea.
Banda yule mgonjwa aliyefanywa zezeta na kaka alieleza kisa chote kwamba alirubuniwa kwa mali za yule mama na akahamishiwa pale kwake. Alisema aliitelekeza familia yake miaka minane iliyopita kabla ya kufanywa zezeta.
Alisema aliwahi kuambiwa kabla tabia ya mwanamke yule lakini maneno ya watu yakawa kama yanaingia na kutokea upande wa pili wa sikio. Alisema anajuta na alimshukuru Bwana Makang’ako kwa ushirikiano alioufanya hadi wakawa watu tena.
Alipopewa nafasi kaka Edgar, hakuzungumza lolote alikuwa akibubunjikwa na machozi hadi mshereheshaji alipomnyang’anya kipaza sauti nafasi ikawa yangu lakini mimi niliomba kaka Ipacho aseme ambapo aliwashukuru wote hasa Bwana Makang’ako aliyewezesha mazoezi yote ya kupatikana kwa ndugu hao na kupona kabisa kwa gharama zake.
“Hili jambo liwe fundisho kwa wanaume wanaopenda vya bure, yaani kulishwa na wanawake matajiri bila kufanya kazi. Wote wenye tabia hiyo wajifunze kutokana na waliyoyapata hawa ndugu zangu,” nilisema na kukafuatia na makofi.
* * *
Tulisafiri kwa ndege asubuhi nikiwa mimi, kaka Ipacho na kaka Edgar kuja Dar kutoka Lilongwe, Malawi. Tulipofika nyumbani, tulikuta baba ametuandalia sherehe kubwa, nikawasimulia jinsi yule mwanamke alivyomfanya kaka yangu zezeta mwanzo- mwisho. Wazazi, ndugu na jamaa walilia kilio cha furaha.
Mwisho.
Umejifunza jambo? Tuma SMS.
Wiki ijayo, Tulivyoteseka Kwenye Mianzi ya Nangose.