
Kampuni ya simu za mkononi ya Halotel hapa nchini imetoa msaada wa vifaa mbalimbali vya masomo kwa waalimu na wanafunzi wa shule ya sekondari Bonyokwa ili kupunguza changamoto za mahitaji ya vifaa vya elimu zinazowakabili.
Akitoa taarifa hiyo leo wakati wa kukabidhi vifaa hivyo katika shule hiyo Jijini Dar es salaam, Mkuu wa Kitengo cha Bidhaa na Mawasiliano wa Kampuni hiyo, Sakina Makabu, amesema wameamua kusaidia vifaa hivyo kutokana na changamoto zinazozikabili shule hiyo.

Aidha, Sakina amesema mpango huo ni kuunga mkono juhudi za serikali ambazo zimekuwa katika kuhakikisha shule zote nchini zinapata mahitaji na vifaa muhimu vitakavyowezesha wanafunzi kupata elimu katika mazingira bora ili kukuza kiwango cha ufaulu wa wanafunzi hao na katika kupunguza uhaba wa vifaa vya elimu kwa shule zote nchini.
“Halotel tumeamua kutoa msaada huu wa vifaa ambavyo ni meza na viti vya waalimu, kabati la vitabu na mafile, desktop mbili na printer ikiwa ni mojawapo ya muitikio wa kampuni yetu wa kuitikia juhudi za serikali katika uboreshaji wa mazingira na upatikanaji wa vifaa vya ufundishaji na kujifunzia ili kuongeza ufanisi wa kufundishia na kujifunzia katika mfumo wa nadharia na vitendo”. Aliongeza Sakina.

Pamoja na hilo, Halotel inatoa huduma ya kimasomo ijulikanayo kama ‘Halostudy’ itakayowawezesha wanafunzi nchini kusoma masomo yao kwa njia ya mtandao (TEHAMA) inayopatikana kwenye simu za mkononi na kwenye kompyuta ambapo wanafunzi na walimu kote nchini wanatumia bure,hivyo kupitia kompyuta tulizotoa leo Shule ya Bonyokwa itaweza kutumia huduma hii kitakachohitajika tu ni kuwa na internet kwenye kompyuta hizi.

Kwa upande wake Mkuu wa shule ya sekondari Bonyokwa Bi Upendo William Mgaza alisema, “ Tumefarijika sana kwa kupokea msaada huu kutoka Kampuni ya simu ya Halotel, tunawashukuru sana kwa kuendelea kuwa karibu na jamii na kuthamini lakini pia kwa kuunga mkono jitihada za kuisaidia sekta ya elimu nchini. Ninaamini kabisa vifaa hivi vitawasaidia walimu na wanafunzi hapa shuleni katika kuboresha namna ya ufusnishaji na kujifunza kwa ujumla”.
Aidha, Diwani ya kata Bonyokwa Mhe: Tumike Jabir Malilo, aliipongeza kampuni ya simu ya Halotel kwa hatua hii ya kuisaidia shule hii na kuunga mkono juhudi za serikali kwa sababu bado ni changa na ina uhitaji mkubwa sana wa vifaa kwaajili ya kufundisha na kujifunzia ili kuweza kukuza kiwango cha utoaji elimu shuleni hapo, ambapo wanatarajia kupokea wanafunzi wapya wa kidato cha kwanza.
Halotel itaendelea kushirikiana na serikali pamoja na wadau wengine wa elimu katika kuhakikisha wanafanikisha uitoaji elimu na inasonga mbele na kutengeneza wanafunzi bora wanaosoma masomo ya sayansi hasa kuelekea ukuaji wa uchumi wa viwanda.