×

Mwanafunzi Ajeruhiwa Vibaya na Fisi

Wambua David, mwanafunzi wa darasa la nne katika Shule ya Msingi Yindundu iliyopo Mtito Andei Kaunti ya Makueni nchini Kenya amenusurika kifo baada ya kuvamiwa na fisi akiwa shambani na kujeruhiwa vibaya.

 

Kwa mujibu wa mama wa kijana huyo, Esther Ndinda mwanaye amefikwa na mkasa huo Jumatatu ya Desemba 20, 2021 ambapo akiwa shambani, alivamiwa na fisi huyo na kumjeruhi vibaya kichwani na miguuni na sasa anaendelea na kupatiwa matibabu katika Hospitali ya AMREF Kibwezi.

 

Kwa mujibu wa mashuhuda, baada ya kijana huyo kuvamiwa na fisi, alijaribu kupiga kelele za kuomba msaada, zilizowakusanya majirani ambao walifika na kutoa msaada wa haraka wa kumuwahisha hospitali, huku jitihada za kumsaka fisi huyo zikigonga mwamba.

 

Akizungumza wakati akiendelea na matibabu wodini, Wambua amewashukuru majirani waliowahi kufika eneo la tukio kutoa msaada ambao ndiyo waliomuokoa asipate madhara zaidi kutoka kwa fisi huyo anayedhaniwa kuwa ametoroka katika mbuga ya wanyama ya Tsavo Magharibi.

 

Daktari Mkuu wa hospitali ya AMREF Kibwezi, Dkt. James Mbui aliyeongoza harakati za kuokoa maisha ya kijana huyo, amesema hali ya Wambua inaendelea kuimarika baada ya kufanyiwa upasuaji kwenye majeraha yake na kueleza kuwa kumekuwa na visa kadhaa vya wakazi wa eneo hilo kuvamiwa na wanyamapori.

 

Hili ni tukio la pili la fisi kuvamia kijiji hicho ambapo siku kadhaa zilizopita, fisi mwingine alivamia kijiji hicho na kuua zaidi ya mbuzi na kondoo 20 huku wengine wakijeruhiwa.

Leave a Comment