
UPO uwezekano mkubwa wa Yanga kuvunja benki na kwenda kumnunua kipa wa St George ya Ethiopia,
Charles Lukwago ambaye ni kipa namba moja wa Timu ya Taifa ya Uganda ‘The Cranes’.
Hiyo ikiwa ni siku chache Yanga itangaze kuhitaji kipa atakayechukua nafasi ya Djigui Diarra raia wa Mali anayetarajiwa kwenda kwenye Michuano ya Kombe la Afrika (AFCON 2021) nchini Cameroon.
Awali ilielezwa Yanga ipo katika mipango ya kumsajili kipa namba moja wa Ruvu Shooting, Mohammed Makaka na
Aboutwalib Mshery wa Mtibwa Sugar.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Spoti Xtra, Kocha Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi amekataa kipa mzawa
atakayekuja kuchukua nafasi ya Diarra na badala yake anataka wa kigeni.

Mtoa taarifa huyo alisema kipa anayepigiwa chapuo la kuja kuchukua nafasi ya Diarra ni Lukwago ambaye
amependekezwa na benchi la ufundi, huku kiungo Khalid Aucho akihusishwa katika usajili huo.
Aliongeza kuwa mabosi wa Yanga tayari wamemfuata kipa huyo kwa ajili ya kuanza mazungumzo ya awali kwa
ajili ya kukamilisha usajili wake kipindi hiki cha usajili wa dirisha dogo.
“Uongozi unafahamu kabisa kuhusiana na Diarra kuwa Januari, mwakani hatakuwa sehemu ya kikosi
chetu kutokana na majukumu ya timu ya taifa ya Mali aliyokuwa nayo.
“Hivyo haraka uongozi umechukua uamuzi wa kumtafuta mbadala wake, awali kocha alipanga kusajili kipa
mzawa.
“Lakini hivi karibuni alibadili uamuzi kwa kuomba asajiliwe kipa kutoka nje ya nchi mwenye uwezo mkubwa
wa kudaka na pendekezo la kwanza lilikuwa kwa kipa namba moja wa timu ya taifa ya Uganda ambaye ni Lukwago,” alisema mtoa taarifa huyo
WILBERT MOLANDI NA MUSA MATEJA, Dar