
KOCHA Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi, amewapa majukumu mazito wachezaji wake akiwemo winga mpya, Chico Ushindi kwa kuwaambia wahakikishe wanapata matokeo mazuri ya ushindi katika kila mchezo uliopo mbele yao.
Yanga ambayo inaongoza Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi 32 baada ya kucheza mechi 12, ndiyo timu pekee hadi sasa ndani ya ligi hiyo ambayo haijapoteza mechi.
Nafasi ya pili kwenye msimamo inakamatwa na Simba yenye pointi 24 kabla ya jana Jumamosi kucheza na Mtibwa Sugar.
Leo Jumapili, Yanga itakuwa mgeni wa Polisi Tanzania katika mchezo wa Ligi kuu Bara utakaochezwa Uwanja
wa Shekh Amri Abeid, Arusha.

Akizungumza na Spoti Xtra, Nabi alisema bado wana safari ndefu ya kuelekea kwenye ubingwa licha ya kuendelea kupata matokeo mazuri kila kukicha, lakini amewataka wachezaji wake kuendelea kupambana kuhakikisha hawatoki nje ya mstari.
“Kitu kikubwa ambacho bado tunapaswa kukiangalia ni jinsi ya kuendelea kupata matokeo ya ushindi katika kila
mchezo ambao upo mbele yetu kwa sababu ni jukumu la kila mchezaji kuhakikisha tunapata matokeo ya kufikia
malengo ya ubingwa.
“Presha bado kubwa kwa sababu bado tuna mechi nyingi kwa kuwa hakuna ambaye amefikia nusu ya ligi, hivyo ni
jukumu la kila mchezaji ambaye anapata nafasi ya kucheza kuhakikisha anatoa alichonacho ili kufikia malengo ya
kupata matokeo mazuri kutokana na ugumu wa ligi yenyewe,” alisema Nabi.
STORI: IBRAHIM MUSSA, DAR ES SALAAM