
Dar es Salaam: 26 Januari 2021: Benki ya Exim Tanzania imetangaza washindi wa promosheni yake inayojulikana kama “Weka Mkwanja tukutoe!” ambapo taasisi ya Work of Mary (Focolare Movement Tanzania) ya mkoani Iringa iliibuka mshindi wa zawadi kuu gari aina ya Toyota Vanguard kwenye kampeni hiyo iliyolenga kuhamasisha wateja wake kujiwekea akiba.
Mbali na taasisi hiyo washindi wengine sita (6) waliweza kujishindia zawadi ya fedha taslimu mil 1 kila mmoja katika droo hiyo iliyofanyika makao makuu ya benki hiyo jijini Dar es Salaam kwa usimamizi wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha nchini pamoja na wawakilishi wa vyombo vya habari pamoja na maofisa mbalimbali wa benki hiyo.

Washindi waliojinyakulia zawadi ya fedha taslimu ni pamoja na Didas Patrick Moshi, SN Partners Architects Limited, Amirali Hassanali Alarakhia/Tahir Amir Alarakhia, Fatna Saleh Tambwe, Stewart Emmanuel Kinunda na Peter Tulizo Sewa ambao walizawadiwa fedha kiasi cha sh Mil 1 kila mmoja.
Akizungumza wakati wa droo hiyo, Mkuu wa idara ya wateja wadogo na kati Benki ya Exim Bw Andrew Lyimo alisema kupitia kampeni hiyo mbali na gari hiyo jumla ya fedha kiasi cha sh mil 18 zilitolewa kwa washindi wapatao 18 ambapo pia benki hiyo imeweza kuongeza mtandao zaidi wa wateja wapya huku pia ikifanikiwa kuhamasisha wateja waliokuwepo awali kujiwekea akiba zaidi.
“Katika promosheni hii iliyodumu kwa kipindi cha miezi mitatu, wateja wetu wa awali na wale wapya waliofanya miamala kuanzia kiasi cha sh laki tano (500,000) na kuendelea, waliweza kuingia moja kwa moja kwenye droo kubwa ya kujishindia gari yaina Toyota Vanguard pamoja fedha taslimu kiasim cha sh mil 1 kila kwa kila mshindi,’’

“Huu ulikuwa ni muendelezo wa utamaduni wa benki ya Exim katika kutoa zawadi bora na faida kwa wateja wetu huku wakati huo huo tukiendelea kutoa huduma bora za kibenki.’’ Alisem Lyimo.
Kwa mujibu wa Bw. Lymo kampeni hiyo ya “Weka mkwanja tukutoe” haikuwasaidia tu wateja wao kujijengea utamaduni wa kujiwekea akiba bali pia imewazawadia kwa jitihada hizo.
“Tunafurahia kuwazadawadia washindi wa promosheni ya“Weka mkwanja tukutoe” na matumaini yetu kuwa watawavutia wengine kuanza kujijengea utamaduni wa kujiwekea akiba. Tutaendelea kujenga tabia ya kuweka akiba nchini ambapo tutawasaidia wateja wetu kutimiza malengo ya muda mrefu na mfupi kwa kujiunga na benki yetu” alisema.