
Benki ya Exim Tanzania hii leo imeungana na Dunia kwa ujumla katika kusherehekea Siku ya Wanawake Duniani. Katika kuadhimisha siku hiyo muhimu viongozi waandamizi wa benki hiyo wakiongozwa na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki hiyo Bw Jaffari Matundu walipata fursa ya kufurahi pamoja na kujadili mambo mbalimbali na wafanyakazi wa benki hiyo ikiwemo kuhamasisha usawa wa kijinsia katika uendeshaji wa benki hiyo.

Katika mazungumzo yake na wafanyakazi hao Bw Matundu alisema benki hiyo inachukulia kwa umuhimu mkubwa suala la usawa wa kijinsia sambamba na kuwawezesha wanawake katika nyanja mbalimbali ikiwemo suala zima la ajira.

“Kipaumbele kwa wanawake katika benki ya Exim hakiishii tu kwa wafanyakazi wetu bali pia wateja wetu. Tumekuwa tukifanya jitihada za makusudi katika kuinua ustawi wa wanawake kupitia huduma zetu tunazozitoa ikiwemo mikopo na mafunzo ya kibiashara,’’ alisema.



