×

Putin Azipiga Mkwara Mzito Nchi Za Magharibi

RAIS wa Urusi, Vladimir Putin kupitia njia ya runinga ameyapiga mkwara mzito mataifa ya Magharibi huku Marekani akiwa mlengwa mkuu kutokana na kile anachokiita ni malengo ya kutaka kuwagawa wananchi wa Urusi dhidi ya propaganda zao za kutaka kuitawala dunia.

 

Putin ameonya kwa kusema kuwa harakati za mataifa ya Magharibi na Marekani kutaka kuitawala dunia zinaelekea kufikia ukingoni, lakini pia amewaonya matajiri wa Urusi ambao wanaisaliti nchi yao kwa kufuata ushawishi wa mrengo wa Marekani na mataifa ya Jumuiya ya Umoja wa Ulaya (EU) ambao amedai wana nia ovu ya kuiangamiza Urusi kwamba hatawaacha salama.

 

“Sitaki kuwahukumu hao wenye majengo Miami au Ufaransa, ambao wanaishi kwa kula vizuri lakini tatizo ni kwamba wanaishi huko na si huku, ni watu wetu na watu wa Urusi,” alisema Putin.

 

“Mataifa ya Magharibi yatajaribu kwa kuwashawishi wasaliti wa nchi yetu, kuigawa nchi yetu, kuwagawa wananchi wetu, kuhangaika kutimiza malengo yao na kuna lengo moja tu kuiangamiza Urusi.”

 

Putin amesisitiza kuwa mgogoro uliopo kati yake na Ukraine uliandaliwa mapema kama sababu ya nchi za Magharibi kupata kisingizio cha kuiwekea Urusi vikwazo kwani nchi hizo hazipendi kuiona Urusi imara na yenye uhuru lakini pia ameeleza kuwa mapambano nchini Ukraine yanaendelea vizuri na Urusi itatimiza malengo yake katika vita hiyo.

 

Rais Putin amesema kwamba kama mataifa ya Magharibi yanadhani nchi yake itarudi nyuma katika vita hii basi kifupi ni kwamba hawaielewi vizuri Urusi, na amedai kwamba vikwazo vya kiuchumi vinavyowekwa na mataifa ya Magharibi havina nguvu kwa sababu mataifa mengi hayaungi mkono vikwazo hivyo.

 

Licha ya kwamba vikwazo alivyowekewa na mataifa ya Magharibi vinaiathiri nchi yake katika jitihada za kutimiza malengo yake ya kivita nchini Ukraine, Rais Putin amesema zipo jitihada za makusudi zinazofanywa na serikali yake ili kuwasaidia wananchi wake kukabiliana na changamoto hasa ya ukosefu wa ajira pamoja na ongezeko la bei za bidhaa.

 

Leave a Comment