
Waziri wa ardhi nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula ametoa onyo kwa wananchi na makampuni yanayovamia maeneo ya wazi na makazi kwa nia ovu ya kudai fidia Kutoka Serikalini ili kujipatia fedha zisizohalali.
Dkt. Mabula ameyasema hayo wakati akizungumza katika mkutano na wananchi wa Keko machungwa kata ya chang’ombe jijini Dar es salaam, kwenye utatuzi wa mgogoro wa Ardhi Kati ya wananchi na familia ya Bw. Akida Bi Lupia waliokuwa wakidai kuwa wananchi hao walivamia maeneo Yao bila uthibitisho rasmi wa mauziano kati Yao na Marehem Bibi yao.

Dkt. Mabula amesisitiza kuwa Ardhi yote ipo chini ya Rais Samia Suluhu Hassan hivyo maeneo yote yaliyomegwa na kurejeshwa kwa wananchi kutokana na kuwa na migogoro yapimwe na kurasmishwa ili wananchi wapate hati za maeneo Yao kwa ajili ya matumizi mbalimbali ya maendeleo.
Waziri Dkt. Mabula aliongozana na viongozi mbalimbali akiwemo Kamishina msaidizi wa Ardhi mkoa wa Dar es salaam Ndugu Idrisa Kayera na watumishi wengine wa Wizara hiyo

Baada ya kusikiliza pande zote mbili zilizokuwa zikirumbana, Dkt. Mabula aliamuru eneo hilo lipimwe na kurasmishwa maramoja ili wananchi wapate hati zao na kuwa wamiliki halali wa viwanja vyao wanavyoishi kwa sasa.

Kwa upande wao Wananchi walitoa shukrani zao kwa Waziri kwa maamzi aliyoyafanya na hawakusita pia kumshukuru Rais wa jamhuri ya muungano mama Samia Suluhu Hassan kwa utendaji wake uliotukuka katika Kuleta maendeleo ya nchi na wananchi Wake.