
REUBEN Mtitu maarufu kwa jina la Mzee Kisangani ambaye ni mbunifu wa kuyeyusha chuma katika eneo la Mkiu wilaya ya Ludewa mkoani Njombe, ameiomba serikali kumsaidia ili aweze kufika nchi zilizobobea katika uyeyushaji wa chuma kujifunza zaidi utaalamu kutokana na uwezo alionao.
Mjasiliamali huyu mwenye umri wa takribani miaka 60 anayefanya shughuli mbambali mkoani Njombe ikiwemo kilimo cha Parachichi,kutengeneza zana zinazotokana na Chuma pamoja na kuyeyusha chuma.
Ametoa ombi hilo alipotembelelewa na waandishi wa habari katika eneo lake la kuyeyusha chuma lililopo wilayani Ludewa.
“Niombe serikali iweze kunipeleka nchi zilizobobea kwenye uyeyushaji wa vyuma nikaone angalau mara moja tu kuwa wao wamefikia wapi angalau na mimi niweze kuanzia pale kwasababu kitu ninachofanya hapa sijatazama kwa mtu ni kitu ambacho nimebuni mwenyewe”alisema Kisangani.
Aidha licha ya ombi hilo Mzee Kisangani ameishukuru serikali kupitia waziri wa madini Dotto Biteko kwa kumtembelea katika eneo lake miaka kadhaa iliyopita na kutoa ahadi kadhaa ambazo baadhi ya ahadi hizo ziliweza kutekelezwa.
Miongoni mwa ahadi zilizofikiwa ni makaa yam awe kwa ajili ya moto kutumia kuyeyusha chuma ambapo mzee huyo amesema licha ya kupata mkaa huo lakini pia ameweza kuufanyia utafiti zaidi.

“Mkaa huu ni mzuri sana lakini nimeufanyia utafiti zaidi,huu mkaa niligundua una moshi na aina fulani ya mafuta.
Nikafanya utafiti ili kuondoa moshi ili huu mkaa uweze kutumika hata viwanda vya ndani badala ya kununua kutoka china na nimefanikiwa kwa hiyo unaweza kutumika hata maeneo ya makazi”aliongeza Kisangani.