Catarina amelazwa hospitali ya Ocean Road akisumbuliwa na saratani ya damu, ugonjwa ulioibuka ghafla wakati akifuatilia afya ya Kevin, kijana waliyependana lakini hawakuwahi kuelezana ukweli wa mioyo yao.
Kevin hivi sasa anaendelea vizuri na ametoka hospitali na kurejea nyumbani, wazazi wake wamemkatalia kabisa kumuona Catarina ingawa alitaka jambo hili litokee. Matibabu ya mionzi yameanza kwa Catarina na wazazi wake wameelezwa kwamba yanaweza kuwa na madhara lakini inabidi wakubaliane kwani lengo ni kuokoa maisha ya mtoto wao wa pekee.
Je, nini kitaendelea?
SONGA NAYO…
Kazi ya dawa za mionzi au chemotherapy kama zilivyoitwa kwa lugha ya Kiingereza ilikuwa ni kuua chembechembe za saratani mwilini mwa mgonjwa, ndivyo zilivyofanya mwilini mwa Catarina, zilianza kuua chembechembe za saratani taratibu lakini katika kufanya hivyo ziliathiri pia chembechembe nyingine za mwili wake.
Hiyo ilifanya hali yake badala ya kuimarika dawa hizo zilipoanza, idhoofike zaidi!
Akakonda kupindukia, nywele zote zikaisha kichwani, vipindi vya homa vikaongezeka na mara kwa mara akawa anaongezewa damu. Hakuwa na uwezo wa kuongea wala kuwasiliana na mtu yeyote, kwa alivyoonekana akiwa kitandani wakati wowote angeweza kupoteza uhai.
“Kabla hajaanza dawa za mionzi hali yake ilikuwa mbaya lakini si mbaya kama ilivyo sasa, inavyoonekana dawa hizi zinazidi kumuumiza!” ndugu wa baba yake walishauri kila walipoona hali yake inazidi kudidimia.
“Sina la kufanya inabidi nisikilize wanachonieleza madaktari!”
“Hapana, lazima tujiongeze, hatuwezi kubaki hapa tu nashuhudia mtoto akielekea kaburini.”
“Sasa tufanye nini?” mama yake Catarina aliuliza.
“Yuko mtaalam mmoja huko Arusha ana uwezo kabisa wa kuponyesha saratani, watu wengi sana wamekwishapona baada ya kutumia dawa zake.”
“Hakuna kitu kama hicho, huo ni uongo tu, tangu lini chembechembe za saratani zikauliwa na dawa za miti shamba? Watu wengi walishajidanganya na kuacha matibabu ya hospitali, mwisho wake hali zao zikawa mbaya wakarejea hospitali wakiwa wamechelewa, mwanangu ana saratani lakini haijasambaa sana, kinachomsumbua hivi sasa ni dawa za mionzi, akizimaliza hizi ataimarika tu!”
“Lakini ungetusikiliza baba Catarina, tunaongea kutokana na uzoefu wetu, sisi tumeiona dunia kabla yako, tunafahamu mambo mengi!” mmoja wa ndugu aliongea akionyesha masikitiko.
“Najua mmeiona dunia kabla yangu lakini sayansi imetoa majibu ya matatizo mengi ambayo huko nyuma yalikuwa hayawezekani, miongoni mwa matatizo hayo ni saratani kama ukiwahi hospitali hakika utapona na Catarina hajachelewa ni bora aendelee na matibabu hapahapa Ocean Road, mengine yote namwachia Mungu!”
Kulikuwa na mvutano mkubwa upande wa familia ya Catarina, wengi wakidai ilifaa aondolewe hospitali kwenda kwenye matibabu ya miti shamba lakini wazazi wake walisimama kidete kupinga uamuzi huo, dawa za mionzi zikaendelea kuingia mwilini mwa Catarina.
Dozi ilitolewa kwa siku tano, kisha kupumzika kwa siku tisa kabla hajawekewa tena dozi nyingine mpaka awamu ya kwanza ya matibabu ikatimia hali yake ikiwa bado ni dhaifu, madaktari wakaagiza kipimo cha kipande cha uboho kichukuliwe kwenye mfupa wake kwa ajili ya kupima ili kuona kama dawa zilikuwa zinasaidia.
Majibu yalipotoka yalionyesha maendeleo kidogo, vipimo vingine zaidi vikafanyika kuangalia figo, moyo, ini na damu yake, ikagundulika mwili ulikuwa umeanza kujiimarisha, ndipo madaktari wakaamua kuendelea na awamu ya pili ya matibabu Catarina akiwa bado hajitambui.
“Msiwe na wasiwasi, kinachomfanya awe na hali hii ni dawa lakini ndani ya mwili wake kuna maendeleo yameanza kuonekana!”
“Kweli daktari?” baba yake Catarina aliuliza.
“Ni kweli, sina sababu ya kukudanganya, naomba tu mniamini!”
“Asante daktari.”
Daktari akawageukia wenzake aliokuwa nao kando ya kitanda na kuwaeleza juu ya hatua ambazo zingefuata kwenye matibabu ya Catarina, wote nyuso zao zilikuwa zikionyesha matumaini ingawa kwa kumuangalia mgonjwa kitandani haikuwa rahisi kuamini angepona, Catarina alishabaki mifupa tupu, nywele zikiwa zimekwisha kichwani, mtu yeyote aliyewahi kumuona siku za nyuma, isingekuwa rahisi kumtambua katika sura aliyokuwa nayo.
“We have finished the induction dose, now we are moving to the consolidation dose with Cytarabine and Amisacrine, broad spectrum anti-biotics and blood transfusion!” (Tumemaliza hatua ya kwanza ya dawa, sasa tunaendelea na hatua ya pili ya kuimarisha ili kuhakikisha chembechembe zilizokufa hazirejei kwa kutumia dawa aina ya Cytarabine na Amiscarine, dawa za kuua wadudu zenye nguvu na pia kumuongezea damu.) Dk. Ngamila aliongea mbele ya kundi la madaktari na madaktari wanafunzi waliokuwa wamemzunguka.
Daktari aliandika maelezo yake yote kwenye faili ya mgonjwa na kilichofuata baada ya hapo ni matibabu kuendelea na dawa alizoziandika, kwa wiki nne mfululizo dawa za mionzi ziliendelea kudondoka kuingia kwenye mishipa ya damu ya Catarina, hakuna mtu aliyeongea habari za Kevin wala haikujulikana alikuwa wapi wakati huo.
***
Hali ya Kevin ailishaimarika kabisa akiwa nyumbani kwao, haikuwa rahisi kuamini alipitia kwenye kipindi kigumu cha kutaka kupoteza uhai, wazazi wake walikuwa wenye furaha mno, wakitembelewa mara kwa mara na wanafunzi wa shule ya sekondari ya St. Joseph waliotaka kufahamu maendeleo ya mwanafunzi mwenzao.
Kitu kimoja kikubwa ambacho Kevin aliwasumbua nacho ni kukutanishwa na Catarina, wazazi wake hawakuwa tayari kumruhusu kutoka nyumbani, alilindwa na kusimamiwa mchana na usiku! Baadaye wazazi wake walipogundua jambo hili lilikuwa likimsumbua sana nafsi, ukizingatia hali yake iliishaimarika, waliamua kulegeza msimamo.
“Kevin!”
“Naam mama!”
“Kesho ni siku yako ya kuzaliwa, unataka tukupe zawadi gani?”
“Catarina!”
“Catarina tu?”
“Ndiyo mama, kama kweli unataka nifurahi, nikutanishe na Catarina, maisha yangu hayawezi kuwa kamili bila mimi kukutana naye, wewe ni mama yangu siwezi kukuficha, nampenda Catarina na siwezi kutenganishwa naye, mnanizuia nisitoke hapa lakini nataka muelewe siku ya kwanza nitakapotoka humu ndani jambo nitakalolifanya ni kumtafuta, sasa kama hivyo ndivyo, kwa nini msinikutanishe naye?” aliongea Kevin macho yake yakilengwalengwa na machozi.
“Usijali, nitashauriana na baba yako!”
“Asante mama.”
Jioni ya siku hiyo baba yake aliporejea kutoka kazini waliketi chini na mkewe kujadiliana, muda mfupi baadaye alitoka tena na kuingia ndani ya gari kisha kuondoka, nyuma mama yake akamfuata Kevin na kumwambia “baba amekwenda kumtafuta!” Ilikuwa ni habari njema mno kwake yeye, akabaki macho mpaka saa sita ya usiku akimsubiri baba yake arudi lakini hakutokea, usingizi ukamchukua.
Alizinduka siku iliyofuata asubuhi saa kumi na mbili na nusu wazazi wake walipoingia chumbani na kuketi kitandani kwake, baada ya salamu ndipo baba yake alimtaarifu kuwa alifanikiwa kumpata Catarina akiwa hospitali ya Ocean Road na wazazi wake, hali yake ikiwa bado ni mbaya.
“Baba naomba nimuone!”
“Amka ujiandae, tunatakiwa kufika hospitali saa moja na nusu, wazazi wake wamekubali tukupeleke!”
Kevin akakurupuka kitandani kuingia bafuni ambako alijimwagia maji si kuoga, kisha akatoka na kujifuta, ndani ya dakika kumi alishamaliza kuvaa na kuteremka hadi chini ambako aliwasubiri wazazi wake, waliposhuka wakatoka wote hadi nje na kuingia ndani ya gari, safari ya moja kwa moja hadi Hospitali ya Ocean Road ambako gari liliegeshwa, wakashuka na kutembea mpaka wodi ya wagonjwa mahututi.
“Shikamoo!” Kevin alimuamkia baba yake Catarina, vivyo hivyo mama yake.
“Marahaba Kevin hujambo?”
“Sijambo, habari za siku? Catarina anaendeleaje?”
“Bado, yupo utamuona!” waliitikia kwa pamoja.
Wazazi walipomaliza kusalimiana ndipo wakaongozana kuingia wodini na kusimama kando ya kitanda, Kevin akiwa ameelekeza macho yake kwa aliyelala juu ya kitanda hicho, alionekana kutoamini alichokuwa akikiona, machozi yakaanza kumbubujika.
“Huyu ni Catarina?” akauliza.
“Ndiyo.”
Akasogea karibu zaidi kisha kuinamisha kichwa chake, akambusu shavuni, machozi yakadondoka na kumlowanisha Catarina ambaye alilala hapo akiwa hajitambui, wazazi wote walishindwa kuyazuia machozi yao, wao pia wakachukua vitambaa na kuanza kujifuta.
“Nini kilimtokea?”
“Aliugua tu!”
“Aliugua nini?”
“Saratani!”
Kevin akageuza tena kichwa chake kumuangalia Catarina, kisha kuusogeza mdogo wake karibu kabisa na sikio na kuanza kunong’ona maneno ambayo hata wazazi wake waliyasikia; Catarina, nakupenda Catarina, hata wewe unafahamu ni kiasi gani nakupenda, kwa muda mrefu nilishindwa kufungua mdomo wangu kukueleza kilichomo moyoni mpaka nilipopata ajali, hata hivyo niliporejewa na fahamu nilisoma daftari lako na kugundua ni kiasi gani unanipenda, nakusihi usikubali kuachia roho yako, ishikilie kwa mikono miwili, usikubali kufa uniache, rejea duniani tufunge ndoa baada ya kumaliza masomo, nakupenda kwa moyo wangu wote!
Alimaliza Kevin, kilichofuata baada ya hapo kilikuwa ni kikohozi kutoka katikati ya kitanda, wote wakasogea karibu, Catarina alikuwa amekohoa na baadaye kufumbua macho, jambo ambalo katika muda mrefu tangu alazwe hospitali lilikuwa halijatokea.
Je, nini kinaendelea? Fuatilia siku ya Ijumaa kwenye gazeti la Championi.