
MSHAMBULIAJI wa Yanga, Fiston Mayele, amesema kuwa deni kubwa alilobakiza kwa sasa ni kuifunga Simba pekee, mara baada ya kumalizana na Namungo kama ambavyo aliwaahidi mashabiki.
Mayele juzi Jumamosi alifanikiwa kuifungia Yanga bao moja katika ushindi wa mabao 2-1 walioupata dhidi ya Namungo FC kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar.
Akizungumza na Championi Jumatatu, mara baada ya kufanikiwa kuifungia Yanga bao hilo, Mayele alisema kuwa katika ahadi ambazo aliziahidi kwa mashabiki, sasa amebaki na deni moja nalo ni kufunga bao katika mchezo wao dhidi ya Simba, Jumamosi ijayo.
“Mashabiki walikuwa wakinidai kuzifunga timu mbili ambazo ni Simba na Namungo, niliweka ahadi hii kwao kwa kuhakikisha kuwa nazifunga hizi timu, nashukuru kuona nimefanikiwa kufanya hivyo dhidi ya Namungo.
“Hivyo kwa sasa nina deni katika mchezo dhidi ya Simba kuhakikisha kuwa nafunga goli (bao) kwa ajili yao, sio rahisi kwa kuwa mabeki hawatakubali kuona nafunga lakini nitapambania hilo,” alisema Mayele.
Stori na Marco Mzumbe