
MSANII wa Bongo Fleva Ali Kiba maarufu kama King Kiba leo Mei 27, 2022 ameongea na waandishi wa habari akiwa maeneo ya Tabata ambapo amegusia suala la kuzindua Kampeni ya Usafi katika maeneo ya Tabata inayotarajiwa kufanyika kesho Mei 28, 2022.
Kampeni hiyo inakwenda kwa jina la Usafi na Kiba, inatarajiwa kwenda sambamba na maonesho mbalimbali ya biashara ambayo yataambatana na fursa mbalimbali za kujifunza namna ya kujiongezea kipato kupitia Mitandao ya Kijamii.
Akiongea na waandishi wa habari Ali kiba amesema anafanya jambo hilo kama hisani huku akishirikiana na wadau mbalimbali ambao anaamini kwa pamoja wanaunga juhudi za Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Amos Makalla katika kuhakikisha kwamba Jiji la Dar es Salaam linakuwa safi na salama.

Kwa upande mwingine Ali Kiba ambaye ni shabiki mkubwa wa soka na shabiki mkubwa wa Klabu ya Yanga amesema Yanga kesho ana zaidi ya asilimia 60 za kushinda mchezo wa nusu fainali ya kwanza ya Kombe la Shirikisho la Azam Sports japo amesema licha ya kwamba timu ya Simba haijawa katika ubora wake msimu huu lakini inabaki kuwa mpinzani mzuri wa Yanga.
King Kiba amewatoa hofu wapenzi wa soka pamoja na burudani ya muziki kuwa maandalizi yapo sawa jukwaa linafungwa na kesho kutakuwa na burudani ya kila aina ikichagizwa na huduma mbalimbali za vyakula na vinywaji lakini pia mechi zote kubwa ya Yanga na Simba pamoja na Fainali ya Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya kati ya Liverpool na Real Madrid nayo itaoneshwa mubashara katika maeneo hayo ya Tabata.