×

Kwa Mwanangu Nitakayemzaa – 38

ILIPOISHIA:

Destiny ameshafuzu kuwa mwandishi wa habari, yuko Kenya akitokea Marekani alikokuwa kimasomo tayari kuzianza harakati zake za kumbadilisha Mtima kijana aliyempenda sana, kwa upande wa kijana huyo na rafiki yake Abdulrahman walizidi kusababisha maafa makubwa kwa kufanya mauaji ya kutisha sehemu tofauti ndani ya nchi ya Somalia na Kenya.TAMBAA NAYO…

TUKIO walilofanya Mtima na Abdulrahman katika kituo cha kulelea watoto yatima kiitwacho Jerusalemu Disabled Children Cares (JDCC), lilimchanganya mno Waziri wa Ulinzi na Usalama Jenerali James Nkoyo.

Ukweli ni kwamba hali ilikuwa inatisha, idadi ya watu waliopoteza maisha ilikuwa ni kubwa kuliko kawaida, jambo la kusikitisha zaidi iliendelea kuongezeka baada ya majeruhi wengine kuendelea kupoteza maisha ambao walikuwa wamelazwa kwenye Hospitali ya Nairobi.

Taarifa hizo zilitangazwa pia kwenye vyombo vya habari, nchi nzima ya Kenya ikagubikwa kwa simanzi na vilio kila kona, watu wakiwalilia ndugu zao waliopoteza maisha na wale waliojeruhiwa.

“Roho inaniuma mno kwa yanayotokea,” mwanamke mmoja alisikika akimwambia mwenziye mtaani.

“Hata mimi, watu wanaokufa hawana hatia, inashangaza kuona serikali inashindwa kuliangamiza kundi hilo.”

Kila mahali nchini Kenya watu walikuwa wanazungumzia juu ya matukio ya Kundi la WAB, hata hivyo ilifikia hatua wananchi wakaingia mtaani na kuanza kuandamana wakimtaka waziri wa ulinzi kuachia madaraka.

Suala hilo likampa hasira sana waziri huyo wa ulinzi ambaye kabla ya cheo hicho aliwahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Nairobi, Naibu Waziri wa Nishati na Madini na Waziri wa Ardhi na Mipango ya Maendeleo, hapo Kenya.

Akapania kufanya juu chini kuhakikisha anarejesha heshima yake ambapo kupitia vyombo vya habari alitangaza siku tisini za kuhakikisha anaviangamiza vikundi vyote vya kijasusi nchini humo.

Habari hizo zilivuma kama upepo, kupitia vyanzo vyao vya taarifa Mtima na Abdulrahman walizinasa wakiwa katika Msitu wa Aachan uliopo nje ya mji wa Garbahrey walikokuwa wamejichimbia. Lakini hata hazikuwashtua!

Ukweli ni kwamba dhamira yao ilikuwa ni kuhakikisha dunia nzima inatambua na kukubaliana na msemo wa Kiswahili usemao ukiua kwa upanga na wewe utauawa kwa upanga. Kwa imani waliyokuwa wanaiamini hawakuona kabisa tofauti ya mtu anayeitwa mlemavu wa ngozi (albino) na binadamu wa kawaida.

Kwao waliwachukulia binadamu wote kuwa sawa na Mtima aliuhesabu ulemavu wake wa ngozi kuwa sawa na ulemavu wa mikono, miguu au hata macho ambapo kwa jamii si jambo la ajabu.

Waliendelea na maongezi yao lakini jambo la kushangaza, bila kutegemea tukio walilofanya kwenye kituo cha kulelea watoto yatima cha JDCC lilikuwa linajirudiarudia kwenye akili ya Mtima, ambapo lilionekana kumsumbua lakini alijitahidi kupambana na hali hiyo.

Saa zikasonga mbele lakini usiku wakiwa wamelala Mtima alijikuta akiota ndoto iliyomtisha sana!

Aliota yuko ndani ya msitu mnene wenye giza zito akikimbizwa na kundi la watu wenye asili ya Kiarabu wenye silaha mikononi.

Aliendelea kuzidi kukimbia akiwa mwenye wasiwasi mkubwa hadi mbele zaidi alikokuta kuna njia mbili, iliyoenda kushoto na nyingine kulia.

Kwa haraka huku watu wale wakizidi kumkaribia aliwaza akimbilie njia ipi akaamua aelekee kushoto, lakini alipotaka tu kwenda huko, alisikia sauti ya mtoto mdogo ikimuita kutoka upande wa kulia.

Mtima hakupuuzia, akaamua kumfuata mtoto huyo, aliyemuuliza kwa nini alikuwa anakimbia kisha baada ya Mtima kumuelezea, mtoto huyo alimuonesha sehemu ya kujificha huku akimhakikishia kuwa ilikuwa ni sehemu salama.

Akiwa mwenye wasiwasi mwingi huku akionekana haamini kilichotokea mara lile kundi la watu lilifika mahali pale, lilipotaka tu kumdhuru yule mtoto alimfunika kwa mikono yake na kutoa sauti kali, ikiuliza; “Kwa nini mnataka kumtendea unyama mtu asiye na hatia?” Baada ya swali hilo, Mtima alishtuka alipokuwa amelala!
Je, nini kitaendelea? Usikose wiki ijayo.

Leave a Comment